Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Ahl al-Bayt (A.S) - Abna -: Dokta Masoud Pezeshkian, Jumapili usiku, katika Sherehe ya 30 ya kuwatukuza na kuwakirimu wahudumu wa Qur'an Tukufu, akizungumzia nafasi ya Qur'an katika mwongozo wa kibinafsi na wa kijamii, alisema: Leo hii katika jamii yetu, kuna watu wengi wanaohifadhi na kusoma Qur'an, na idadi yao inaongezeka siku baada ya siku. Hii ni neema kubwa na inaonyesha juhudi za wapenzi wanaofanya kazi katika mwelekeo wa kufundisha na kueneza elimu na maarifa ya Qur’an, lakini jambo linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba, uwepo wa Qur’an katika jamii haukomei tu katika kuhifadhi na kusoma (Qur'an), bali inapaswa kuonekana katika matendo na mtindo wetu wa maisha.
Akirejea Aya ya Qur'an isemayo: (إِنَّ هَٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ / "Hakika Qur'an hii inaongoza katika yaliyonyooka kabisa"), Rais amebainisha: Aya hii inasema (katika maana yake) kuwa Qur’an inaongoza kwenye njia iliyo imara na iliyo bora zaidi, lakini ikiwa tunaichukulia Qur’ani kuwa ni nuru, inakuwaje sisi bado ni wanyonge katika nyanja nyingi katika jamii zetu? Kwa nini tukabiliane na changamoto katika Sayansi, Maadili, tabia (Akhlaq) na Usimamizi?.
Akisisitiza umuhimu wa kuunganisha maarifa ya Qur'an na mazoezi ya kijamii, Dk. Pezeshkian alisema: Tatizo kubwa ni pengo kati ya kuijua na kuitekeleza Qur'an. Tunadai kuwa Qur’an inatuonyesha njia ya uongofu na inamfikisha Mwanadamu katika kilele cha juu zaidi, lakini ikiwa kivitendo hakuna dalili ya mwongozo huu inayoweza kuonekana katika maisha yetu ya kibinafsi na ya kijamii, basi kwa hakika tunapaswa kuangalia upya tabia zetu.
Akizungumzia ulazima wa kuwepo kwa maelewano kati ya elimu ya Qur'an na mtindo wa maisha, Rais alibainisha: Haiwezi kudaiwa kuwa Qur'an inamulika njia, lakini kukawa kuna jamii ambayo ina changamoto katika Usimamizi, Maadili, Uadilifu wa Kijamii na Tabia (Akhlaq). Ikiwa tunaifahamu Qur'an, lakini hatuitumii kivitendo, hii inaashiria uwepo wa pengo kubwa linalohitaji kujazwa (kuzibwa).
Akizungumzia Tafsiri ya Imamu Sadiq (amani iwe juu yake) kuhusu uongofu na njia ya maisha, Dokta Pezeshkian amesema: Imesemwa katika Hadithi kwamba ikiwa Waislamu watazingatia Aya mbili tu za Qur’an, basi wanaweza kupata njia sahihi ya maisha yao na kufika sehemu wanayoingojea (na kuitarajia). Aya hizi mbili zinasema: (لَآ إِلَٰهَ إِلَّا ٱللَّهُ / Hapana Mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja", (فَبَشِّرْ عِبَادِ، الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ ۚ أُولَٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّهُ ۖ وَأُولَٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ / Wape bishara nzuri waja wangu wanao sikiliza kauli na wakaifuata iliyo bora na yenye kuwaongoa kwendea katika Haki. Hao tu, si wenginewe, ndio Mwenyezi Mungu atao wafikisha kwenye Uwongofu. Na hao tu, si wenginewe, ndio wenye akili zilizo nawirika."
Akisisitiza umuhimu wa kusikiliza yaliyo sawa na bora, Rais alibainisha: Aya hii inarejelea kanuni mbili za msingi. Kwanza Mtu asikilize wengine wanasema nini, na ikiwa wanayosema ni ya kweli ayakubali na ikiwa ni ya uongo aukatae bila kuleta mzozo (na mtafaruku wowote), lakini kwa bahati mbaya hatujajifunza kukaa pamoja na kusikilizana maneno yetu sisi kwa sisi. Ikiwa mtu anasema jambo sahihi, unapaswa kusikiliza (jambo hilo), na ikiwa halikubaliki, unaweza kutokulikubali (na kulikataa), lakini bila kupigana na kufanya uharibifu.
Dk. Pezeshkian akirejea Aya nyingine ya Qur’an, inayowazungumzia wale wanaokadhibisha jambo bila ya kuwa na elimu nalo na kuikanusha kwa kutojua (بَلْ كَذَّبُوا بِمَا لَمْ يُحِيطُوا بِعِلْمِهِ وَلَمَّا يَأْتِهِمْ تَأْوِيلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ ۖ فَانْظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ/ Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile. Basi angalia jinsi ulivyo kuwa mwisho wa madhaalimu hao" (Surat Yunus: Aya 39).
Aya hii inawazungumzia wale wanaokadhibisha ukweli na uhakika, bila ya kujua wala kuufahamu ukweli wanaukanusha tu. Hii ndio hatima ile ile mbaya ambayo madhalimu waliotangulia pia walikumbana nayo. Hakuna ukatili mkubwa zaidi ya kwamba mtu anakanusha kitu ambacho hakijui, kwa sababu tu ya ujinga na chuki.
Akikazia kwamba hakuna mtu anayeweza kuepuka hukumu ya ki-Mungu, Rais alisema: Sisi sote ni waja wa Mwenyezi Mungu, na mwishowe, hakuna njia ya kuepuka hihukumu ya ki_Mungu. Ucha Mungu ni bahari ya maarifa ambayo tunapaswa kutiririka nayo katika tabia na maamuzi yetu (tunayoyachukua).
Mwishoni, Dk. Pezeshkian alitoa shukrani zake kwa juhudi na jitihada za waandaaji wa sherehe hii akisema: Ninawashukuru ninyi nyote mnaofanya kazi katika mwelekeo huu.
Katika Mwezi huu uliobarikiwa wa Ramadhani na mikesha hii yenye thamani kubwa, namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie tuwe miongoni mwa watekelezaji wa Qur'an kwa vitendo, tusiwaaibishe Mashahidi na wakubwa wetu, na atujaalie kufaulu kusonga mbele katika njia ya haki na ubinadamu.
Ikumbukwe kwamba Maonyesho ya 32 ya Kimataifa ya Qur'an Tukufu yalianza tarehe 5 Machi, 2025 katika Msikiti wa Imam Khomeini (RA). Maonyesho haya yamefanyika karibia na eneo la karibu mita za mraba elfu 20 na katika sehemu (vipengele) 37.
Your Comment