"Jina langu ni Mahmoud Khalil, na mimi ni mfungwa wa kisiasa," amesema Khalil katika barua iliyochapishwa jana Jumanne. "Kukamatwa kwangu ni matokeo ya moja kwa moja ya kutumia haki yangu ya uhuru wa kujieleza, kwa sababu nimetetea 'Palestine Huru' na kutaka kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza, ambayo yalianza tena kwa nguvu Jumatatu usiku," aliongeza katika barua hiyo, akimaanisha mashambulizi mapya ya anga ya Israel huko Gaza ambayo mamlaka za eneo hilo zinasema yameua zaidi ya Wapalestina 400.
Mawakili wa Khalil wametoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja, wakieleza kuwa alipata kibali cha mkaazi halali wa kudumu wa Marekani mwaka jana. Mkewe ana ujauzito wa miezi minane.
Kukamatwa Mmarekani huyo mwenye asili ya Palestina mnamo Machi 8 kulizua maandamano katika miji mbalimbali ya Marekani, ikiwa ni pamoja yale ya jiji la New York jana Jumanne, wakati mamia walipokusanyika Times Square wakitaka aachiliwe huru.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameapa kuwafukuza nchini humo wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina walioshiriki katika maandamano ya Chuo Kikuu cha Columbia kupinga vita na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza. Trump anadai kuwa "waandamanaji hao wana chuki dhidi ya Wayahudi na wanaunga mkono wanamgambo wa Hamas."
Kinyume chake, watetezi wa Palestina, yakiwemo baadhi ya makundi ya Kiyahudi, wanasema wakosoaji wao wanachanganya kimakosa baina ya ukosoaji wa mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza na chuki dhidi ya Wayahudi, na uungaji mkono wao kwa haki za Wapalestina na eti kuunga mkono wanamgambo wa Hamas.
Wakati huo huo, zaidi ya wabunge 100 wa chama cha Democratic wamehoji uhalali wa kuwekwa kizuizini Mahmoud Khalil katika barua iliyotumwa kwa utawala wa Trump.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, kesi ya Khalil inawakilisha mtihani kwa mahakama za Marekani kuhusu jinsi ya kuainisha uhuru wa kujieleza unaodhaminiwa kwa raia chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani.
342/
Your Comment