22 Machi 2025 - 17:25
Hezbollah: Hatuna uhusiano wowote na shambulio la kombora

Kwa kutoa taarifa rasmi, Hezbollah ya Lebanon imekanusha uhusiano wowote na operesheni hiyo ya makombora leo asubuhi (Jumamosi) dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kusisitiza kuwa, madai ya adui yanalenga kutoa visingizio vya kuendelea na uvamizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahl al-Bayt (a.s) - Abna -; Hezbollah ya Lebanon imetoa taarifa dakika chache zilizopita ikikanusha uhusiano wowote na urushaji wa maroketi kutoka Kusini mwa Lebanon hadi maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.

Taarifa hii inaongeza kuwa: Hezbollah inasisitiza juu ya kushikamana na mapatano ya usitishaji vita na kuiunga mkono Serikali katika kutatua mienendo hiyo ya mvutano ya utawala wa Kizayuni.

Wakati huo huo, Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon amebainisha: Israel imekiuka makubaliano ya usitishaji vita na azimio nambari 1701 la Umoja wa Mataifa zaidi ya mara 1,500, huku Lebanon na Muqawamah (Upinzani) wakiwa wamefuata kikamilifu makubaliano hayo.

Vyanzo vya lugha ya Kiebrania vimeripoti asubuhi ya leo (Jumamosi) shambulio la kombora kutoka kusini mwa Lebanon hadi Kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Vyanzo hivi vilithibitisha kwamba milipuko ilisikika katika mji wa Al Matla, karibu na mpaka wa Lebanon, baada ya ving'ora viwili vya tahadhari kusikika.

Duru za Kizayuni zimeripoti kuwa, roketi 5 zilirushwa kutoka Lebanon kuelekea mji wa Al-Matla, ulioko Kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Vyombo vya habari vya Israel vilitangaza kwamba mfumo wa ulinzi ulinasa makombora matatu kati ya haya.

Baada ya shambulio hilo la kombora, ndege ze kivita za utawala wa Kizayuni zililenga maeneo ya Al-Kharibah, miinuko ya eneo la Al-Tuffah, karibu na mji wa Kfar Houneh, Jabal Jabour na Kfarkela nchini Lebanon.

Duru za Lebanon zimeripoti kuuawa Shahidi watu wawili na kujeruhiwa raia watatu katika hujuma ya utawala wa Kizayuni katikati mwa mji wa Touline Kusini mwa Lebanon.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha