22 Machi 2025 - 21:22
Source: Parstoday
Kofi kali; Jibu la taifa la Iran kwa uhabithi wa Marekani

Akizungumza jana Ijumaa katika kikao na maelfu ya watu wa matabaka tofauti katika siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani wa 1404 Hijria Shamsia, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiogopi vitisho vya Marekani, na kwamba iwapo italisababishia madhara yoyote taifa la Iran, itapata kipigo na kofi kali.

Matamshi hayo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yana umuhimu mkubwa katika pande mbalimbali za ndani na nje ya Iran. Katika upande wa nje, tunaweza kutaja sehemu tatu muhimu zilizoashiriwa katika hotuba ya Imam Khamenei. Sehemu ya kwanza ni mwamko na utambuzi wa mataifa ya dunia kuhusu dhulma na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Palestina kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi na hasa Marekani. Utawala wa Kizayuni uliendesha vita vilivyodumu kwa muda wa miezi 15 dhidi ya watu wasio na hatia wa  Ukanda wa Gaza na kufanya mauaji ya halaiki ya wazi, ya makusudi na yaliyopangwa mapema dhidi ya watu hao madhulumu.

Ijapokuwa viongozi wa Kizayuni wanadai kuwa wameshinda vita kwa sababu ya ugaidi na mauaji ya halaiki waliyoyafanya dhidi ya wakazi wa Gaza, lakini moja ya matokeo muhimu na ya wazi ya vita hivyo ni kuongezeka mwamko, hasira na kuchukizwa mataifa ya dunia na jinai zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na utawala habithi wa Israel unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, dhidi ya Wapalestina. Suala hili lilitiliwa mkazo katika hotuba ya jana ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Akiashiria hasira hiyo ya kimataifa kuhusu jinai za utawala katili wa Israel, Ayatullah Khamenei amesema, hii leo uhabithi wa utawala katili wa Kizayuni umeumiza nyoyo za mataifa mengi, hata yale yasiyo ya Kiislamu.

Kofi kali; Jibu la taifa la Iran kwa uhabithi wa Marekani

Sehemu ya pili ya hotuba hiyo ilihusu kuwakumbusha Wamarekani na watu wa Ulaya kuhusu makosa wanayoyafanya kuhusiana na makundi ya muqawama. Wamarekani na Wazungu yaani watu wa Ulaya, wamedai mara kwa mara kwamba makundi ya muqawama ni makundi yanayopigana na kuendesha mapambano kwa niaba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Licha ya Iran kuyaunga mkono kikamilifu makundi hayo ya muqawama lakini imetangaza wazi kuwa haina makundi yoyote ya niaba yanayopigana kwa ajili yake. Katika hotuba yake ya siku ya kwanza ya mwaka wa 1404 Hijria Shamsia, Ayatullah Khamenei ameitaja tafsiri ya wanasiasa wa Marekani na Ulaya kuhusu makundi ya muqawama kwa kuyatuhumu kuwa ni makundi ya niaba, na kusisitiza kuwa hilo ni kosa kubwa na hatua ya kuyavunjia heshima. Amehoji: "Niaba ni kitu gani? Wananchi wa Yemen na vituo vya muqawama katika eneo hili wana msukumo wa ndani wa kusimama dhidi ya Wazayuni, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haihitaji naibu wala mwakilishi, na mtazamo wetu na mtazamo wao unajulikana wazi."

Sehemu ya tatu ya kimataifa katika hotuba ya jana ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jibu lake kwa  vitisho vya hivi karibuni vya watawala wa Marekani, hasa Rais Donald Trump wa nchi hiyo.

Trump, ambaye ameingia Ikulu ya White House kwa mara ya pili, anazungumza kuhusu kufanya mazungumzo na Iran kwa upande mmoja, na kuitishia kwa upande mwingine akidai kwamba ikiwa Iran haitakuwa tayari kufanya mazungumzo, italazimika kubeba matokeo ya uamuzi wake huo. Kwa maneno mengine ni kwamba Trump anaitishia Iran kuwa atatumia nguvu za kijeshi dhidi yake iwapo haitakubali kufanya mazungumzo chini ya mashinikizo na vikwazo. Mtazamo wa Trump ni kwamba anaweza kufikia malengo yake kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kutumia lugha ya mabavu na vitisho. Kuhusiana na hilo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake ya jana ameichukulia lugha ya vitisho dhidi ya taifa kubwa na shupavu la Iran kuwa ni lugha isiyo na tija na iliyofeli.  Huku akisisitiza kuwa, Wamarekani wanapaswa kutambua vizuri kwamba, hawatafika popote kwa kutumia vitisho dhidi ya Iran, Ayatullah Khamenei ametilia mkazo suala hilo kwa kusema: Wao na wengine wafahamu kuwa wakilifanyia uhabithi taifa la Iran, watazabwa makofi makali.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha