22 Machi 2025 - 21:28
Source: Parstoday
Mwangwi wa matamshi ya Imam Khamenei katika vyombo vya habari duniani

Matamshi yaliyotolewa jana na Kiongozi Muadhamu wa mapinduzi ya Kislamu, Imam Ali Khamenei katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Hijria Shamsia akijibu vitisho vya Rais wa Marekani, Donald Trump, yameakisiwa kwa mapana na marefu katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Katika hotuba yake mbele ya umati mkubwa wa wananchi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliionya Marekani dhidi ya kutumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, maadui watazabwa kofi kali la usoni iwapo watafanya kitendo chochote kiovu dhidi ya Iran.

Shirika la habari la Ufaransa (FP), limeiweka kauli za Kiongozi Muadhamu juu kabisa ya habari zake na kuandika: Ayatullah Khamenei ametangaza kwamba Marekani haitafika popote kwa kuitishia Iran.
Chombo hiki cha habari cha Magharibi kimetathmini matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni jibu kwa vitisho vya Rais wa Marekani, Donald Trump, vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Tehran.

Mwangwi wa matamshi ya Imam Khamenei katika vyombo vya habari duniani

Shirika la habari la Reuters limehusisha kichwa cha ripoti yake na kauli za Kiongozi Muadhamu kuhusu kujitegemea kwa harakati za Muqawama na mapambano na kuandika: Kiongozi wa Iran ametangaza kuwa Wahouthi wa Yemen wanafanya kazi kwa kujitegemea.

Shirika la habari la Reuters limeashiria matamshi ya Trump kuhusu uwajibikaji wa Iran katika operesheni za Ansarullah nchini Yemen na kuongeza kuwa: "Uongozi wa Iran umesema kuwa, Wahouthi wa Yemen wanafanya kazi kwa msukumo na maoni yao binafsi, na Tehran haihitaji nguvu ya niaba katika eneo hilo."

Gazeti la Kizayuni la "Jerusalem Post" pia limechagua kichwa cha habari "Kofi Kali" kwa ajili ya kuakisi matamshi ya Ayatullah Khamenei na kuandika: "Kiongozi wa Iran ameitishia Marekani."

Mwangwi wa matamshi ya Imam Khamenei katika vyombo vya habari duniani

Shirika la habari la kimataifa la Bloomberg limeakisi kauli ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuandika: "Wakati Iran inatayarisha jibu la barua ya Trump, imepinga vitisho vya Marekani."

Bloomberg imeandika: Kiongozi wa Iran ameapa kujibu uchokozi wowote wa Marekani kwa kofi kali, lakini ametangaza kuwa Iran haitaanzisha vita.

Tovuti ya Palestine Online pia imeakisi sehemu ya matamshi ya Imam Ali Khamenei na kusisitiza kuwa: Taifa la Iran limemshinda adui katika njama zake kadhaa. Hapana shaka kwamba matokeo ya mwisho ya misimamo hii itakuwa kushindwa kwa adui na utawala mbovu, fisadi na mbaya wa Kizayuni.

Na Tovuti ya "Al-Wasat" ya Libya pia imeandika kuwa, baada ya vitisho vya Donald Trump vya uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Iran, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Vitisho vya Marekani dhidi ya Iran kamwe havitafika popote."

Katika matamshi yake ya jana mbele ya umati mkubwa wa wananchi mjini Tehran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena alisisitiza katika kujibu vitisho vya maadui wa Iran kwamba: "Hatujawahi kuanzisha vita na mapigano, lakini iwapo mtu yeyote ataanzisha mapigano kwa chuki, ajue kwamba atazabwa makofi makali."

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha