Carpenter ametoa indhari hiyo kwa rais wa Marekani katika makala iliyochapishwa kwenye jarida analolihariri la The American Conservative.
Mchambuzi huyo wa masuala ya ulinzi na sera za nje amemhutubu Trump kwa kumwambia: "vita na Iran havitakuwa kama wanamitindo wanaotembea katika maonyesho ya mitindo".
Akiashiria chokochoko zinazofanywa na maseneta wa Marekani wenye misimamo mikali, wanaomchochea Trump juu ya suala hilo, Carpenter ameeleza kwenye makala yake hiyo kwamba, watu wenye msimamo mkali wamejaribu kupuuza maonyo yanayotolewa, kwamba uingiliaji wa kijeshi unaweza kusababisha hatari ya kuanza vita vingine visivyo na mwisho katika Asia Magharibi.
Carpenter, ambaye pia ni Profesa na mhadhiri wa taaluma za ulinzi na sera za nje katika Taasisi ya Cato ameashiria madai ya Trump kwamba vita hivyo havitadumu kwa muda mrefu na vitamaanisha kuangamizwa Iran na akasema: "majigambo ya aina hii yanakumbusha kauli za Kenneth Edelman, aliyekuwa naibu wa waziri wa zamani wa ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld, kabla ya Vita vya Iraq mwaka 2003".
Akilifafanua hilo mchambuzi huyo amesema: "Edelman alitabiri kwamba vita vya kumpindua Saddam Hussein, dikteta mwendazake wa Iraq, vitakuwa kama 'wanamitindo wanaotembea kwenye jukwaa la maonyesho ya mitindo', lakini utabiri wake haukutimia, na zaidi ya wanajeshi elfu nne wa Marekani walipoteza maisha katika vita hivyo".
Mchambuzi huyo wa Kimarekani ameongezea kwa kusema: "kuna sababu kadhaa zinazoonyesha kuwa vita dhidi ya Iran havitakuwa sawa na utembeaji wa wanamitindo kwenye jukwaa la maonyesho ya mitindo. Kufanya hivyo kwa matarajio kuwa shambulio la gharama ndogo na la umwagaji mdogo wa damu litaleta ushindi wa uhakika na wa haraka kwa Marekani kunamaanisha jinsi wachukuaji maamuzi walivyofikia kwenye kilele cha upumbavu. Serikali ya Trump inapaswa ijiepushe na kutumbukia kwenye shimo kama hilo".
Trump, ambaye yeye mwenyewe alikiuka mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA yaliyofikiwa mwaka 2015 kwa kuitoa Marekani kwenye makubaliano hayo miaka mitatu baadaye katika mwaka 2018, siku hizi amekuwa akitumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran katika harakati zake za kujaribu kuishawishi Jamhuri ya Kiislamu ifanye mazungumzo na Washington.../
342/
Your Comment