Katika taarifa fupi, Idara ya Wakfu za Kiislamu katika mji mtukufu wa Quds imesema, waumini wapatao 180,000 walisali Isha na Tarawehe katika usiku wa siku ya 26 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwenye Msikiti wa Al-Aqsa, kwa ajili ya maandalizi ya Lailatul-Qadr.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waumini hao walifanikiwa kufika msikitini hapo licha ya ukweli kwamba utawala ghasibu wa Israel umeugeuza mji wa Baitul Muqaddas kuwa eneo la kijeshi na kuweka vizuizi vikali kwa wale wanaofika kwenye Msikiti wa Al-Aqsa kuingojea Lailatul-Qadr.
Kituo cha Habari cha Wadi Hilweh, ambayo ni taasisi ya kutetea haki za binadamu katika mji wa Quds kimesema, "idadi kadhaa ya wale waliopigwa marufuku kuingia Msikiti wa Al-Aqsa walisali Sala ya Isha na Tarawehe nje kidogo ya milango ya msikiti".
Hayo yanajiri huku utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa umewazuia Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi wenye umri wa chini ya miaka 55 kwa wanaume na miaka 50 kwa wanawake kuingia katika mji wa Baitul Muqaddas ili wasiweze kusali katika Msikiti wa Al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.
Usiku wa kuamkia mwezi 27 Ramadhani una umuhimu maalumu kwa Waislamu, ukiwa ni moja ya mikesha 10 ya mwisho ya mwezi, ambapo waumini hupitisha muda wa usiku kucha katika Sala kuanzia baada ya Sala ya Isha mpaka unapoingia wakati wa adhana ya Sala ya Alfajiri.../
342/
Your Comment