28 Machi 2025 - 09:49
Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Itrah wangu, Ahlul-Bayt wangu au Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Hadithi sahihi na iliyothibitishwa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni yenye lafdhi hii isemayo: «وأهل بیتي» / "Na Ahlul-Bayt wangu”, ama riwaya ile ambayo imepachikwa lafdhi au neno «وسنّتي» / “Na Sunna yangu” badala ya lafdhi ya asili na sahihi isemayo: «وأهل بیتي» / "Na Ahlul-Bayt wangu”, riwaya hiyo ni batili kwa mtazamo wa sanadi ya upokezi wa Hadithi husika.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-: Hadithi sahihi na iliyothibitishwa kutoka kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni yenye lafdhi hii isemayo: 
«وأهل بیتي» / "Na Ahlul-Bayt wangu”, ama riwaya ile ambayo imepachikwa lafdhi au neno «وسنّتي» /  “Na Sunna yangu” badala ya lafdhi ya asili na sahihi isemayo:

«وأهل بیتي» / "Na Ahlul-Bayt wangu”, riwaya hiyo ni batili kwa mtazamo wa sanadi ya upokezi wa Hadithi husika. Na sasa hebu tunazungumzie nyaraka sahihi za maandiko yote mawili (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu) / (وسنتي/ Na Sunna yangu) ili kuweka wazi kwa kila mtu aweze kutambua kwamba hati sahihi ya Hadithi isemayo:  (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu) ina uhalali kamili na usahihi, tofauti na hati nyingine ile ambayo imekataliwa kabisa na ni batili tena ubatili wake uko bayana na wazi kuliko hata uwazi wa jua kali la utosi.

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Sanadi ya Hadithi isemayo: (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu)

Nakala (Matni) ya Hadithi hii yenye lafdhi hii (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu), imenukuliwa na wasimuliaji wakuu wawili wanaokubalika sana kwa Masunni kupita maelezo, na ni hawa kama ifuatavyo:

1- Sahihi Muslim

Muslim, katika Sahih yake, anasimulia kutoka kwa bwana wetu Zayd bin Arqam, radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, anasema: Siku moja, Mtume wa Mwenyezi Mungu - s.a.w.w - alitoa Khutba karibu na bonde la maji liitwalo "Khum" lililopo kati ya Makka na Madina; Katika yake alimtukuza Mwenyezi Mungu na akawausia watu, kisha akasema:

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

«أیُّهَا النّاسُ! فَاِنَّما أنَا بَشَر یُوشَكُ أنْ یَاْتِيَ رَسُولُ رَبّي فاُجیبَ، وَأنَا تارِك فِیکُمْ ثِقْلَیْن: أوَّلُهُما کِتابَ اللهِ فِیهِ الْهُدی وَالنُّور، فَخُذُوا بِکتابِ اللهِ وَاسْتَمْسکُوا به» فحثّ علی کتاب الله ورغّب فیه ثمّ قال:

«وَ أهل بَیْتي، أذکّرکُمُ الله فِي أهْل بَیْتِي، أذکّرکُمُ الله في أهْل بَیْتي، أذکّرکُمُ الله في أهل بَیْتي».

"Fahamuni enyi watu! Hakika Mimi ni Mwanadamu, anakaribia Mjumbe wa Mola wangu kunijia nami ni niitike wito wake, nami nimewaachia vizito viwili: Cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho ndani yake kuna uongofu na nuru, chukueni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mshikamane nacho", Mtume akasisitiza zaidi juu ya kukifuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kisha akasema: "Na (Ahlul-Bayt wangu) watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu".

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Hebu hapa tutumie akili timamu kuzingatia sentensi hii: ("Nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu"), Mtume Muhammad (s.a.w.w) alirudia sentensi hii mara tatu!.

Kurudia mara tatu sio kwamba alikuwa amekosa kazi za kufanya, kwamba anarudia bila makusudio yoyote! Hapana, kuna falsafa yake na maana yake ni pana sana, tunachoweza kukisema hapa ni kwamba huo ni msisitizo wa hali ya juu na kuonyesha umuhimu mkubwa wa Umma wake kushikamana na Ahlul-Bayt wake (amani iwe juu yao) baada yake, na sio kuishia kusema ooh, hata sisi tunawapenda Ahlul-Bayt! Kuwapenda kivipi yaani? unawapendaje wakati wewe huwafuati na uko kinyume nao na hushikamani nao kwa lolote?!, maana sahihi ya kuwapenda Ahlul-Bayt (a.s) ni kushikamana nao na kuwafuata wao na sio wengine, na hii ni kwa Mujibu wa Hadithi hiyo sahihi tuliyoinukuu hapo juu, na uzuri hiyo nukuu imekuja ndani ya Kitabu ambacho kinaitwa Sahih Muslim, kwamba ndio kitabu sahih zaidi baada ya Qur'an!, tizama anuani yenyewe ni Sahih Muslim!.

Kama ni Sahih Muslim, (na unadai kwako wewe hiki ndio kitabu sahihi zaidi na ndio muongozo wako katika vitabu vya Hadithi na Riwaya), maana yake ni hii kwamba: Akili timamu inakuhukumu kwamba, unatakiwa kuelewa maana ya maneno hayo ya Mtume (s.a.w.w) na kuyafuata kikamilifu, ambapo anasema (s.a.w.w): "Nami nimewaachia vizito viwili: Cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu ambacho ndani yake kuna uongofu na nuru, chukueni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mshikamane nacho", Mtume akasisitiza zaidi juu ya kukifuata Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kisha akasema: "Na (Ahlul-Bayt wangu) watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu, nakukumbusheni Mwenyezi Mungu juu ya watu wa nyumba yangu". 

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Sasa ikitokea mtu unabeba Sahih Muslim, ambayo imenukuu maneno hayo ya Mtume (s.a.w.w), na unaita Kitabu hicho kuwa kwako ni Sahih na hakuna Kitabu Sahihi baada ya Qur'an kuliko Sahih Muslim (n.k), lakini bado unakadhibisha maneno hayo na kupingana nayo na kuamua kuwafuata na kushikamana na wasiokuwa Ahlul-Bayt wa Mtume Muhammad (a.s), hakuna shaka wewe utakuwa ni mtu wa ajabu sana!, na utakuwa katika kundi la walioghafilika (kama waliovyotajwa Mwenyezi Mungu ndani ya Surat al-A'raf, Aya ya 179), bali utakuwa unaifanyia nafsi yako dhulma kubwa sana!, na sio hilo tu, bali pia afya ya ufahamu wako itakuwa na mgogoro na matatizo makubwa sana!, bali utakuwa huna tofauti yoyote na Punda!, Maana Punda anaweza kubeba mzigo mkubwa wa vitabu lakini hajui kabeba nini na wala hajui ndani ya alichokibeba kuna kitu gani!, bali haipaswi kusitasita kusema maneno haya ya haki kuwa utakuwa sawa na wale aliowakusudia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndani ya Qur'an pindi aliposema:

"مَثَلُ الَّذِينَ حُمِّلُوا التَّوْرَاةَ ثُمَّ لَمْ يَحْمِلُوهَا كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا ۚ بِئْسَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّهِ ۚ وَاللَّهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ"

"Mfano wa waliobeba Taurati, kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa.Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu." (Surat al-Jum'a: Aya ya 5).

Kisha sehemu nyingine Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

"وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنْسِ ۖ لَهُمْ قُلُوبٌ لَا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَا يَسْمَعُونَ بِهَا ۚ أُولَٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ"

"Nahakika tumewaumbia Jahannam Majini wengi na Watu. Wana nyoyo lakini hawafahamu kwazo, na wana macho lakini hawaoni kwayo, na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi; hao ndio walioghafilika." (Surat Al-A'raf: Aya ya 179).

Tukirudi katika Hadithi hiyo ya Thaqalayni tuliyoinukuu hapo huu, kwa hakika Matni yake au hati yake au andiko lake, limenukuliwa hivyo na Muslim katika Sahih yake (1) na vile vile Al-Darimi katika Sunan yake iitwayo Sunan al-Darimi (2), na sanadi zote vitabu hicyo viwili ziko wazi mno kama vile uwazi wa jua kali la utosi, na hakuna dosari au hata mkwaruzo kidogo tu katika sanadi zake.

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

2-Sunan Tirmidhi

Tirmidhi, pia ameisimulia Hadithi hii Tukufu kwa lafdhi isemayo: (وعترتي، أهل بيتي / Na Itrah wangu, Ahlul-Bayt wangu), na maandiko hayo ya Hadithi hiyo ni kama ifuatavyo:

«اِنّي تارِك فِیکُمُ ما اِنْ تَمَسّکْتمْ بِهِ لَنْ تَضِلُّوا بَعْدِي، أحَدُهُما أكْبَرُ مِنَ الآخَرِ: كِتابُ اللّهِ حَبْلٌ مَمْدودٌ مِنَ السَّماءِ إلَى الأرضِ، وعِتْرَتي أهلُ بَيْتي، لَنْ یَفْتَرِقا حَتّی یَرِدا عَلَيَّ الْحَوض، فَانْظُروُا کَیْفَ تَخْلِفُونِي فِیها».

“Hakika nimekuachieni Vizito viwili, ambavyo mkashikamana navyo, hamtopotea baada yangu, kimoja wapo ni kikubwa kuliko kingine, Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kamba iliyonyooka kutoka mbinguni mpaka ardhini, na itrah wangu (Kizazi changu), Ahlul-Bayt wangu (Watu wa Nyumba yangu). Viwili hivi havitatengana (havita ikhtilafiana) mpaka vitakaponijia huko kwenye (chemchemi) hodhi (ya Kawthar, yaani: Peponi), basi angalieni ni namna gani mtanifuata katika hivyo" (3).

Maneno haya hayako wazi mno na ni rahisi kueleweka. Na ikiwa kuna mtu atadai kuwa hayaelewi, basi ni maneno gani tena mengine yasokuwa hayo yanayoweza kuwa wazi kuliko hayo ili aweze kuyaelewa?!. Mtu akisema mimi siyaelewi maneno haya ya Mtume (s.a.w.w), tatizo litakuwa sio maneno haya, bali tatizo ni mtu mwenyewe tu kwamba ana moyo lakini hawafahamu kwa moyo huyo, na ana macho lakini hawaoni kwayo, na ana masikio, lakini hawasikii kwayo.

Na hapo ndio Mwenyezi Mungu anaposema kwamba: "Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi; hao ndio walioghafilika." (Surat Al-A'raf: Aya ya 179). 

Kwa hakika, hakuna uwazi kuliko uwazi huu uliopo katika Hadithi hii anayoinukuu Tirmidhi. Na nitakuwa ni mtu wa ajabu sana ikiwa nitadai kuwa namkubali Tirmidhi na ninaikubali Sunan Tirmidhi (kwamba ni Kitabu sahih kabisa baada ya Qur'an, natembea nacho kila sehemu na kunukuu yaliyomo ndani yake kwa watu), lakini nikifika katika nukuu ya hadithi, najisafanya sielewi! au nakula nyoya, na kuamua kuficha ukweli huo kwa watu, na kujitoa rasmi akili huku nikujua kuwa huu ndio ukweli halisi na hii ndio haki yenyewe, lakini ili mradi tu niendelee kufuata na kushikamana zangu na njia isiyotajwa katika Hadithi hii!.

Kwa hakika tabia hii imekewa vikali ndani ya Qur'an Tukufu, maana ni kuficha haki unayoijua kuwa hii ndio haki, lakini kwa kufuata matamanio ya nafsi yako unaamua tu kuficha haki ukidhani unaweza kufanikiwa daima kuificha, hakuna aliyeweza hapa duniani kuinyonga haki na akafanikiwa kuinyonga, Mayahudi walijaribu kuinyonga haki na wakajifanya hawamjui wala kumtambua Mtume Muhammad (s.a.w.w), lakini hatima yao ilikuwaje? walifanikiwa?, Ulimwengu kote Mtume Muhammad (s.a.w.w) anatajwa kila kona, hebu tutizame na tuzingatie asemavyo Mwenyezi Mungu (swt) katika Aya hii Tukufu:

"الَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْرِفُونَهُ كَمَا يَعْرِفُونَ أَبْنَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّ فَرِيقًا مِنْهُمْ لَيَكْتُمُونَ الْحَقَّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ"

"Wale tuliowapa Kitabu wanamjua yeye (Mtume) kama wanavyowajua watoto wao. Na hakika kundi katika wao wanaificha haki na hali wanaijua". (Surat Al-Baqarah: Aya ya 146). 

Nukuu hizi mbili (za Muslim na Tirmidhi) kunako Maandiko au Matni ya Hadithi Tukufu ya Thaqalayni, zote zinasisitiza juu ya neno au lafdhi isemayo:  (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu). Na kwa hakika, nukuu hizi mbili zinatosha katika kuthibitisha suala hili,  na sanadi za nukuu zote mbili ni kamili na kamilifu, na hazihitajii hata punje ya utafiti wala majadiliano (maana usahihi wa sanadi zake ni wa kiwango cha juu, hata uamue kuzitaftia dosari ya aina yoyote huipati).

Na kwa kuongeza katika hilo,  wasimuliaji au wahadithiaji au walionukuu Hadithi hii kwa nukuu hizo mbili ndani ya vitabu vyao, ni waandishi wa kile kinachoitwa: Sahih Muslim na Sunan Tirmidhi, ambao wana itibari kubwa na maalum katika ulimwengu wa Ahlu-Sunna. Nani katika Masunni hamkubali Muslim? Kama yupo anyoshe kidole juu?, Na hakuna shaka kama yupo basi huyo atakuwa ni Sunni wa kuchovya!, na vile vile nani asiyemkubali Tirmidhi baina ya Masunni?. Anyoshe kidole juu aseme mimi ni sunni lakini simkubali Tirmidhi?!. Kama yupo huyo sio Sunni halisi, bali atakuwa ni Sunni wa michongo michongo (bandia)!.

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Sanadi ya lafdhi feki isemayo: "  «وَسُنّتی» / "Wa Sunnati" / "Na Sunna yangu"

Riwaya ambayo ndani yake neno hilo «وَسُنّتی» / "Wa Sunnati" / "Na Sunna yangu" limetajwa badala ya (وأهل بيتي / Na Ahlul-Bayt wangu), ni riwaya au hadithi feki na ya kutunga, ambayo pamoja na udhaifu wa mnyororo, au silsila au (sanadi) wa waokezaji wake, riwaya hiyo iliundwa kwa makusudi na kuenezwa (kwa kasi ya hali ya juu mithili ya kasi ya mwendokasi) na mawakala wenye mafungamano na Bani Umaiyya. Sasa hebu tutizame na tutafiti sanadi yake kama ifuatavyo:

Sanadi ya kwanza kwa mujibu wa Masimulizi ya Hakim

Hakim Neishaburi alinukuu Maandiko  ya Hadithi hiyo (isemayo:«وَسُنّتی» / "Wa Sunnati" ) yaliyotajwa katika Mustadrak kwa Sanadi hii tunayoipitia hapa chini:

1.(Abbas) Ibn Abi Uwais, kutoka kwa:
2.Abi Uwais, kutoka kwa:
3.Thaur bin Zaid Al-Dailami, kutoka kwa:
4.Ikrima, kutoka kwa:
5.Ibn Abbas, kwamba Mtume (s.a.w.w) alisema:

«یا أیُّهَا النّاسُ اِنّي قَدْ ترَکْتُ فِیکُمْ، اِنِ اعْتَصَمْتُم بِهِ فَلَنْ تَضِلُّوا أبَداً کتاب الله وَسنّة نَبِیّه».

"Enyi watu, hakika mimi nimeacha kati yenu mambo mawili, Maadamu mtashikilia viwili hivyo, hamtapotea kamwe baada yangu: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake".(4).

-

Rejea:

1.Muslim, Sahih: Juzuu ya 4, Ukurasa wa 3, 18, Namba ya hadithi: 2408, katika chapa iliyochapishwa na Abdul Baqi.

2. Al-Darimi , Sunan: Juzuuya 2. Ukurasa wa 431, na 432.

3. Tirmidhi, Sunan: Juzuu ya 5. Ukurasa wa 663, Namba ya hadithi: 37788.

4. Hakim, al-Mustadrak: Juzuu ya 1. Ukurasa wa 93.

-

Majanga ya Sanadi ya Matni au Maandiko haya ya Hadithi ni  haya kwamba: Ndani ya sanadi kuna Baba na Mwana wanaoonekana mwanzoni mwa Sanadi. Yaani:
1-Ismail bin Abi Uwais.
2-Abu Uwais. 

Baba na Mtoto sio tu kwamba hawajathibitishwa (kuwa wao ni Thiqa katika kunukuu hadithi), bali wanashutumiwa wazi wazi kwa uwongo, uzushi na kughushi hadithi. Sasa hebu tusiandikie mate, tunukuu kauli za wanavyuoni mbalimbali Sayansi (Elimu) ya Rijal, ili tumakate mzizi wa fitina kama ifuatavyo:

(a) Al-Hafidh al-Mizzi, katika kitabu chake "Tahdhib al-Kamal fi Asma al-Rijal" kuhusu Ismail na baba yake, ananukuu yafuatayo kutoka kwa watafiti wa Fani ya elimu ya Rijal:

(b) Yahya bin Mu’in (ambaye ni mmoja wa wanachuoni wakubwa wa elimu ya Rijal) anasema: Abu Uwais na Mwanawe ni dhaifu, na Yahya bin Mu’in amenukuliwa akisema kuwa watu hawa wawili walikuwa wakiiba Hadithi, na Ibn Mu’in pia alisema kuhusu Mtoto (wa Abu Uwais): Hawezi kuaminika (kuaminiwa).

(c) Kuhusu (Ismail) Mtoto wa Abu Uwais, Nasa'i alisema kwamba yeye ni dhaifu na si mwaminifu (haaminiwi). Abul Qasim La'lkai alisema kwamba Nasa'i ilizungumza mengi dhidi yake kiasi kwamba alisema kwamba Hadithi yake inapaswa kuachwa.

(d) Ibn Adi (mmoja wa wanavyuoni wa elimu ya Rijal) anasema: Ibn Abi Uwais anasimulia hadithi za ajabu kutoka kwa ami yake Malik ambazo hakuna anayezikubali. (1).

(e) Ibn Hajar katika utangulizi wa Fat'hu al-Bari anasema: Mtu hawezi kamwe kutolea hoja (kuitumia kama hoja) hadithi ya Ibn Abi Uwais, kwa sababu ya udhaifishaji ambao Nasa'i alifanya juu yake. (2).

(f) Hafidh Sayyid Ahmad bin al-Sadiq katika kitabu chake Fat'hu al-Mulk al-A'li anasimulia kutoka kwa Salama bin Shabib kwamba alimsikia Ismail bin Abi Uwais akisema: “Watu wa Madina wanapogawanyika katika makundi mawili kuhusiana na suala fulani, mimi hughushi hadithi. (3).

Kwa hiyo, mtoto (Ismail bin Abi Uwais), anayetuhumiwa kughushi Hadithi, na Ibn Mu’in akamhusisha na uwongo; hawezi kamwe kukubaliwa mapokezi yake, mtu yeyote mwenye elimu na maarifa ya elimu ya rijali, hawezi kukubali hadithi yoyote ambayo ndani ya sanadi yake yumo ndani yake. Mbali na hayo, Hadithi yake haikutajwa hata moja katika Sahih yoyote ile ya Muslim na Tirmidhi na vitabu vingine vilivyo sahihi.

Kuhusu baba (yake), inatosha kwamba Abu Hatam al-Razi anasema katika kitabu chake kiitwacho “Al-Jarḥ wa al-Ta'dil ( الجَرح والتَعدیل)”: Hadithi yake inaandikwa lakini haifai kutumika kama hoja, na hadithi yake haina nguvu na si madhubuti. (4).

Rejea:

1. Hafidh Al-Mizzi, Tahdhib al-Kamal: Juzuu ya 3. Ukurasa wa 127.

2.Ibn Hajar l-Asqalani, Utangulizi wa Fat'hu al-Ba'ri, Ukurasa wa 391, Chapa ya Dar Al-Maarifa.

3.Hafidh Sayyid Ahmad, Fat'hu al-Mulk al-A'li, Ukurasa wa 15.

4.Abu Hatam al-Razi, al-Jarh wal Ta'dil, Juzuu ya 5. Ukurasa wa 92.

Ni ipi kati ya ibara hizi mbili iliyo sahihi? "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Irah wangu,Ahlul-Bayt wangu" au "Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna yangu"

Hitimisho:

Kwa mantiki hiyo basi, Masimulizi (Riwaya) yoyote ambayo katika Sanadi yake kuna watu hawa wawili, kamwe hayatakuwa na yatakuwa sio sahihi; Mbali na hayo, ni kinyume na riwaya sahihi na thabiti (iliyotajwa na kunukuliwa ndani ya Sahih Muslim na Sunan Tirmidhi).

Sanadi ya pili, na ya tatu ya hadithi hii feki, nazo vile vile ni dhaifu, na maulamaa wengi wa Ahlu - Sunna wameweka wazi udhaifu wake pasina kupepesa macho kama tulivyo ona katika Sanadi hiyo ya kwanza.

Imeandaliwa na kuandikwa na: Ustadhi Taqee Zachalia Othman

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha