"Hakika tutajibu hatua za Marekani, nchi hiyo haitaweza kamwe kuidhoofisha Canada," amesema Carney na kuongeza kuwa, ushuru utawaumiza zaidi Wamarekani kwa muda mrefu, kuliko Canada.
Katika muhula wa pili wa urais wa Donald Trump, Marekani kwa mara nyingine imechukua mkondo wa kuutishia ulimwengu. Kuhusiana na suala hili, Trump bila aibu, ameibua madai mbalimbali ya kutaka kutwaa au kuunganisha Canada, Greenland na Panama na ardhi ya Marekani, na wakati huo huo ameanzisha vita vya kibiashara sio tu dhidi ya washindani wa Washington, hasa China, bali pia dhidi ya washirika wa Marekani kama vile Canada, Mexico na Umoja wa Ulaya. Mtazamo wa kibabe na kichokozi wa Trump umewafanya hata washirika wa karibu sana wa Marekani, kama Canada, kusema waziwazi kwamba hawaiamini tena Washington.
Katika mkutano na waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, katikati ya Machi 2025, Donald Trump alikariri vitisho vyake dhidi ya Canada na kusisitiza nia yake ya kuiunganisha nchi hiyo na Marekani. Trump alidai katika mkutano huo kwamba Canada "imeivamia" Marekani kwa miaka mingi na kwamba hatalegeza kamba katika suala la kuongeza ushuru unaotozwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka ardhi ya Canada. Vilevile alikariri madai yake ya kutaka Canada iuanganishwe na Marekani na kuwa jimbo la 51 la nchi hiyo.
Rais wa Marekani pia amesisitiza mara kwa mara haja ya kukitwaa kisiwa cha Greenland. Hata hivyo watu wa Greenland wamepinga vikali matakwa hayo ya kijuba ya utawala wa Trump. Kwa mujibu wa uchunguzi mpya wa maoni uliofanyika huko Greenland, ni 6% tu ya watu katika eneo hilo wanaotaka kujiunga na Marekani, na 85% wanapinga mpangp wowote wa kuunganishwa Greenland na Marekani.
Trump pia amekuwa akizungumzia mara kwa mara haja ya utawala wa Marekani kudhibiti Mfereji wa Panama kwa kisingizio cha uwepo wa China huko Panama na ameitishia moja kwa moja serikali ya nchi hiyo, kwa kadiri kwamba serikali ya Panama hatimaye imelazimika kufuta makubaliano ya usimamizi wa Mfereji wa Panama na kampuni ya Hong Kong. Panama imekubaliwa kuwa kampuni ya Marekani ya BlackRock itanunua bandari kuu mbili za Mfereji wa Panama kutoka kwa mmiliki wa Hong Kong kwa mkataba wenye thamani ya dola bilioni 22.8. Hatua hii inalenga kushika udhibiti wa kiuchumi wa Mfereji wa Panama na kupunguza ushawishi wa China katika eneo hilo la kimkakati. Pia, kutokana na mashinikizo ya Marekani, Rais wa Panama, José Raúl Mulino alitangaza mnamo Februari 6, 2025, kwamba amefuta makubaliano ya Njia ya Kiuchumi ya Hariri na China. Alisema sababu ya kuchukua hatua hiyo ni mashinikizo ya Marekani ya kutaka kupunguza ushawishi wa Beijing kwenye Mfereji wa Panama. Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Trump kutishia kwamba "Iwapo Marekani haitadhibiti tena Mfereji wa Panama kutatokea jambo kubwa sana.” Trump hakutosheka na hayo, bali amechukua misimamo ya kustaajabisha kuhusiana na kadhia ya Ukraine, suala ambalo limewaacha bumbuazi washirika wa Washington barani Ulaya. Masuala haya yote kwa pamoja yamezifanya nchi za Ulaya zipoteze imani yao kwa Washington na kwa sababu hii, wanachama wa NATO wa Ulaya wanataka kuimarisha uwezo wa kujitegmea katika masuala ya ulinzi.
Misimamo na kauli za Trump zinaonyesha nia yake ya kulazimisha matakwa ya Marekani kwa nchi zingine katika fremu ya mkakati jumla wa serikali yake, yaani amani kupitia nguvu na mabavu. Jambo hili lina maana ya kuvuruga nidhamu ya kimataifa ya kisiasa, kijiografia, kiuchumi na kibiashara na kuhatarisha amani ya kikanda na kimataifa. Kwa sababu hiyo, wakosoaji wa Donald Trump wanamtuhumu kwa kuwadunisha na kuwadharau washirika wa Marekani na kudhoofisha miungano na Washington. Wanatabiri kwamba, katika kipindi cha utawala wa pili wa Trump, Marekani itakuwa katika hali ya kutengwa itakayosababisha hasara kwa maslahi ya Marekani na amani ya dunia.
342/
Your Comment