Esmail Baqaei amelaani kuendelea mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon ikiwemo jinai ya kigaidi iliyofanywa jana na utawala huo katika eneo la Dhahiya mjini Beirut ambayo imesababisha kuuliwa shahidi raia kadhaa wa Lebanon na kamanda mmoja wa harakati ya Hizbullah na mwanaye.
Israel jana Jumanne ilimuua shahidi kamanda wa harakati Hizbullah, Hassan Ali Bdeir, maarufu kwa jina la Hajj Rabih pamoja na mwanawe wa kiume aliyetajwa kwa jina la Ali katika shambulio la anga dhidi ya makazi ya raia mjini Beirut.
Baqaei amesema hadi sasa utawala wa Kizayuni umekiuka makubaliano ya kusimamisha vita kwa zaidi ya mara elfu mbili na kuendeleza kukiuka umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Lebanon. Amesema: Mashambulizi ya kikatili ya Israel dhidi ya Lebanon ni ukiukaji wa wazi wa kanuni na sheria za kimataifa na za kibinadamu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametaja kutochukua hatua nchi zilizosimamia makubaliano ya kusimamisha mapigano mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni kuwa jambo la kusikitisha na ishara ya kuwa batili ahadi na matamko ya nchi hizo katika uwanja huo.
Vilevile ameeleza kusikitishwa na kimya cha mashirika husika ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mbele ya jinai za kutisha za Israel huko Lebanon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kusema Marekani na waungaji mkono wengine wa Magharibi wa utawala huo ni washiriki katika jinai na ukiukaji wake wa sheria. Baqaei amezihimiza nchi za eneo la Asia Magharibi kuchukua hatua kali zaidi ili kukabiliana na uchokozi wa utawala huo ghasibu.
342/
Your Comment