Televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon imeripoti kuwa ndege ya kivita isiyo na rubani ya Israel ililenga nyumba katika mtaa wa Dalaa kwenye mji wa bandari wa Sidon, uliopo kilomita 48 kusini mwa Beirut.
Hassan Farhat, mwanachama wa Hamas, pamoja na mwanawe, waliripotiwa kuuawa shahidi katika shambulio hilo la anga.
Vikosi vya jeshi la Israel pia vilifanya mashambulizi ya muda mrefu katika maeneo mengine ya kusini mwa Lebanon, ikiwemo miji ya Naqoura na Nabatieh, na kusababisha uharibifu na vifo katika maeneo hayo.
Awali, shambulio la anga la Israel lililenga eneo la Wadi Azza kusini mwa Lebanon.
Shambulio lingine la anga la Israel lililolenga gari karibu na mji wa Bint Jbeil kusini mwa Lebanon lilijeruhi watu wawili Alhamisi asubuhi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon, Youssef Rajji, Alhamisi aliitaka Umoja wa Ulaya kuongeza shinikizo kwa Israel iondoke katika maeneo yote ya Lebanon inayoyakalia kwa mabavu, kusitisha mashambulizi na kuheshimu uhuru wa Lebanon.
Rajji alitoa wito huo wakati wa mazungumzo na Stefano Sannino, mkurugenzi mkuu wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Tume ya Ulaya, aliyeongoza ujumbe wa EU ulioitembelea Beirut.
Waziri huyo amelaani kuendelea kwa uchokozi wa kijeshi wa Israel, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kila siku kusini mwa Lebanon na mashambulizi mapya mjini Beirut.
Rajji pia alitaka Israel iheshimu Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701, na ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya ukiukaji huo.
Israel ililazimika kukubali kusitisha mapigano na Hizbullah kufuatia hasara kubwa ilizopata katika kipindi cha karibu miezi 14 ya mzozo, bila kufanikisha malengo yake dhidi ya Lebanon. Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa Novemba 27.
Tangu kuanza kwa makubaliano hayo, vikosi vya utawala haramu wa Israel vimekuwa vikifanya mashambulizi karibu kila siku dhidi ya Lebanon, na kuvunja mkataba huo wa kusitisha mapigano, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga kote nchini humo.
342/
Your Comment