Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Sheikh Mohammad Abdu, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), Leo hii Ijumaa, akitoa Khutba ya Sala ya Ijumaa ndani ya Masjid Al-Ghadir, Kigogo Post, Dar-es-salaam - Tanzania amesema:
Mwenyezi Mungu Ndiye anayestahiki kuabudiwa kwa Haki. Na hakuna Shaka kuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Waislamu wengi walikuwa wakitekeleza Ibada na kujaa Misikitini na kuhudhuria Darsa mbalimbali ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Maeneo ya anasa na kuchuma dhambi yalifungwa kwa Heshima ya Mwezi huu wa Ramadhan, na hii ni kuonyesha kuwa hata wasiokuwa Waislamu wanaheshimu Mwezi wa Ramadhan na kuwapa fursa Waislamu wafanye Ibada bila kubughudhiwa na maeneo hayo ya starehe za kidunia.
Ramadhan imekuwa ni Chuo kwetu na tumejitunza Kumtii Mwenyezi Mungu ndani yake, kuacha dhambi, kuacha Uongo na kuwa watu wacha Mungu, wasomaji wa Qur'an na tumeiishi Qur'an ndani ya Mwezi huu Mtukufu. Mashindano ya Qur'an yamefanyika kwa wingi ndani yake ili kuhuisha Qur'an.
Tunatakiwa kuhakikisha kuwa ile namna tuliyoishi nayo ndani ya Mwenyezi wa Ramadhani, iwe endelevu hata baada ya Ramadhani.
Kama mtu aliacha Uongo ndani ya Ramadhani, aendelee kujiepusha na Uongo kwa sababu yule ambaye aliogopwa adhabu yake ndani ya Ramadhani ambaye ni Mwenyezi Mungu, yupo pia hata baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Aliyekuwa akifanya Ibada za Usiku ndani ya Ramadhani na mwendo wake ukabadilika na tabia zake kuwa nzuri ndani ya Ramadhan, basi aendelee kuwa na tabia nzuri hivyo hivyo hata baada ya Ramadhan. Na hii ni sehemu ya wito na funzo zuri toka kwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) kwetu, akitaka tuwe na tabia njema muda. Na hiyo ndio Taq'wa / Ucha-Mungu.
Mwenyezi Mungu atuone daima katika maeneo anayotaka kutuona, na asituone katika maeneo ambayo amekataza tusionekane ndani yake.
Your Comment