13 Aprili 2025 - 22:36
Source: Parstoday
Waislamu wauawa India katika maandamano ya kupinga Sheria ya Marekebisho ya Wakfu wa Kiislamu

Watu watatu, akiwamo mtoto mmoja, wameuawa na wengine zaidi ya 100 kukamatwa wakati wa maandamano yaliyofanyika katika jimbo la mashariki mwa India la West Bengal kupinga marekebisho ya Sheria ya Bodi za Wakfu wa Kiislamu.

Serikali ya India inadai kuwa, sheria hiyo, iliyopitishwa na Bunge mwezi Aprili, inalenga kufanya mabaraza ya wakfu ya Kiislamu- ambayo ni miongoni mwa wamiliki wakubwa wa ardhi nchini humo - kuwajibika zaidi na kuwa na uwazi.

Hata hivyo kambi ya upinzani inasema sheria hiyo ni "hujuma" dhidi ya Waislamu milioni 200 walio wachache nchini India.

Afisa wa polisi wa jimbo hilo, Javed Shamim amesema watu watatu akiwemo mtoto mmoja, wameuawa katika maandamano hayo.

Ameongeza kuwa: "Hadi sasa, watu 118 wamekamatwa kuhusiana na ghasia hizo," akibainisha kuwa maafisa wa polisi wasiopungua 15 wamejeruhiwa.

Mabaraza yenye nguvu ya Waqf, ambayo yanasimamia mali za wakfu zinazotolewa na Waislamu, yanamiliki takriban hekta 365,000, milki ya mali isiyohamishika yenye thamani ya mabilioni ya dola.

Kiongozi wa upinzani nchini India, Rahul Gandhi, ameitaja Sheria wa Waqf kuwa ni silaha inayolenga kuwatenga Waislamu na kuingilia sheria na haki zao za kumiliki mali.

Waislamu wauawa India katika maandamano ya kupinga Sheria ya Marekebisho ya Wakfu wa Kiislamu

Ameongeza kuwa suala hilo ni "hujuma" ya wazalendo wa Kihindu dhidi ya "Waislamu kwa wakati huu, ingawa inaweka mfano wa kulenga jamii zingine katika siku zijazo."

Vyama vya upinzani vimeeleza kuwa sheria hiyo ni sehemu ya juhudi za chama cha Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, Bharatiya Janata kwa ajili ya kupata kura za wapiga kura wa Kihindu.

Miongoni mwa vipengee vilivyozusha utata mkubwa vya sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la India, ni kuwaruhusu wasio Waislamu kuteuliwa katika Bodi za Kiislamu za Waqfu, jambo ambalo limeibua wasiwasi kuhusu uhuru wa kidini na haki za kihistoria za Waislamu nchini India.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha