Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul Bayt (a.s) - ABNA - Al Jazeera Qatar imesema: Wananchi wa Morocco kwa kushiriki maandamano 105 yaliyofanyika katika miji 58 ya nchi hiyo, walionyesha uungaji mkono wao kwa watu wanaodhulumiwa wa Ghaza na kulaani mashambulizi ya jeshi la Israel katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wananchi wa Morocco pia wameeleza upinzani wao dhidi ya kuweka nanga kwa meli katika bandari za nchi hiyo zinazoelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa ajili ya kuunga mkono utawala haram wa Kizayuni.
Kuhusiana na hili, redio ya Voice of the Maghreb (Sawt al-Maghrib) iliripoti kwamba mamia ya Wamorocco walifanya maandamano makubwa Siku ya Ijumaa iliyopita, Aprili 18, 2025, karibu na bandari ya Dar El-Libda (Casablanca) kupinga kutia nanga kwa meli ya Nexoe Maersk inayoshukiwa kusafirisha sehemu za ndege ya F-35 hadi Israel.
Waandamanaji hao walidai kupigwa marufuku kwa meli kubwa za kampuni ya kimataifa ya usafirishaji ya Maersk Line katika bandari za Morocco.
Kwa mujibu wa redio ya Sauti ya Maghreb, wanasiasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani kote wameishutumu kampuni ya meli kwa kusafirisha shehena za kijeshi zinazopelekwa Israel.
Kulingana na ripoti hii, vikosi vya usalama vya Morocco vilizuia waandamanaji kufika bandarini kwa kuchukua hatua kali za usalama. Waandamanaji, wakiwemo wafanyakazi wa bandari, walishikilia mabango ya kulaani Kampuni ya Usafirishaji ya Maersk na kuimba nyimbo dhidi ya kampuni hiyo.
Your Comment