27 Aprili 2025 - 22:40
Source: Parstoday
Pezeshkian asisitiza haja ya ushirikiano wa nchi za eneo ili kukabiliana na ugaidi

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuna udharura wa kuwepo na ushirikiano thabiti miongoni mwa nchi za eneo hili, ili kwa pamoja ziweze kupambana na zimwi la ugaidi.

Rais Pezeshkian katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif amesisitiza haja ya kupigwa jeki ushirikiano kati ya nchi za kikanda ili kufanikisha vita hivyo dhidi ya zimwi la ugaidi.

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, matukio ya hivi karibuni katika eneo yameongeza maradufu haja ya kuwepo ushirikiano mkubwa wa kieneo ili kukabiliana na tishio la ugaidi, na kusambaratisha rasilimali za kifedha na silaha za makundi hayo ya kigaidi.

Amesisitiza kuwa, nchi za Asia Magharibi zinapaswa kuelekeza nguvu zao zote katika kuimarisha amani, usalama na utulivu katika eneo hili la kistratejia.

Hali kadhalika, Dakta Pezeshkian amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kusaidia katika upatanishi na kutatua mvutano uliopo kati ya Pakistan na India.

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif  kwa upande wake amesema kuwa, kama ilivyo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Pakistan inasisitiza haja ya kudumishwa amani, utulivu na usalama wa kudumu katika eneo hili.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha