28 Aprili 2025 - 22:46
Source: Parstoday
Kiongozi Muadhamu atoa mkono wa pole kufuatia mripuko 'mchungu' kusini mwa Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa salamu za rambirambi kwa familia zinazoomboleza wahanga wa mripuko "mchungu" katika Bandari ya Shahid Rajaee katika mji wa kusini wa Bandar Abbas, na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kuhusiana na tukio hilo.

Katika ujumbe wake wa rambirambi jana Jumapili, Kiongozi Muadhamu amesema tukio la kutisha la moto katika Bandari ya Shahid Rajaee limelitia taifa zima huzuni na wasiwasi.

Ayatullah Khamenei amewataka maafisa wa vyombo vya usalama na mahakama kuchunguza iwapo kulikuwa na uzembe wowote au vitendo vya makusudi, ambavyo huena vilisababisha maafa hayo, na kuchukua hatua za kisheria zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.

"Maafisa wote lazima wajichukulie kuwa wana jukumu la kuzuia matukio machungu na ya uharibifu (kama haya)", amesema.

Imam Khamenei amewatakia rehema na msamaha wa Mwenyezi Mungu waliopoteza maisha; subira na faraja kwa familia zilizofiwa na wapendwa wao; na afueni ya haraka kwa waliojeruhiwa.

Kiongozi Muadhamu ametoa shukurani zake za dhati kwa watu wote wenye huruma ambao walikuwa tayari kuwachangia damu majeruhi wa mkasa huo.

Kwa akali watu 40 waliuawa na wengine zaidi ya 1,000 kujeruhiwa katika mripuko mkubwa uliokumba bandari ya kontena, ambayo iko katika mji bandari wa Bandar Abbas.

Bandari hiyo hushughulikia tani milioni 80 za bidhaa kila mwaka. Serikali ya Iran imeitangaza leo Jumatatu kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa kufuatia tukio hilo la kusikitisha.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha