19 Mei 2025 - 19:09
Source: Parstoday
Malengo makuu ya utawala wa Trump ya kuandaa mpango wa kuwahamishia Libya Wapalestina

Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, unaendeleza mpango wa kuwahamisha kabisa Wapalestina milioni moja kutoka Ukanda wa Gaza na kuwapeleka Libya barani Afrika.

NBC News imeripoti ikinukuu vyanzo vya habari, kwamba serikali ya Trump inafanyia kazi kwa bidii mpango wa kuwahamisha kabisa Wapalestina milioni moja wanaoishi Gaza na kuwapeleka Libya. Chini ya mpango huo, Marekani intaachilia mabilioni ya dola, mali ya Libya, zinazoshikiliwa nchini humo mkabala wa kuwakubali na kuwapokea Wapalestina.

Mpango huu wa kuwahamisha kabisa Wapalestina milioni moja kutoka kwenye nchi yao, ambao sasa unapendekezwa na serikali ya Trump, unaweza kuonekana kuwa ni mwendelezo wa sera ambayo Marekani na Israel zilikuwa zimeainisha hapo awali kwa jina la kuwahamishia Wapalestina katika ardhi nyingine, mpango ambao ulikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka nchi jirani, nchi nyingi za dunuia na taasisi za kimataifa. Tangazo la mpango mpya wa kuwahamishia Libya watu wa Gaza linaonyesha kuwa serikali ya Trump bado inachunguza njia mbalimbali za kuwafukuza Wapalestina wa Gaza katika nchi yao, na licha ya upinzani wote wa Wapalestina na nchi nyingi za dunia, inasisitiza kutekelezwa mpango huo kama eti moja ya masuluhisho ya kumaliza vita vya Gaza na kutimiza matakwa ya Israel.

Hii ni licha ya kwamba, msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza rasmi kwamba: "Tunapinga mpango wowote wa kulazimishwa Wapalestina kutoka Gaza au aina yoyote ya maangamizi ya kizazi." Wakati huo huo, harakati ya Hamas imesisitiza mara kwa mara haki ya watu wa Palestina kubakia katika ardhi na nchi yao na imepinga vikali mpango wowote wa kuwahamisha au kuwapeleka uhamishoni. Hivi karibuni, Sami Abu Zuhri, kiongozi wa ngazi za juu wa harakati ya Hamas alisema kuwa, matamshi ya mara kwa mara ya Rais wa Marekani kuhusu kulazimishwa Wapalestina wa Gaza kuyahama makazi ya yao kwa visingizio kama vile kujengwa upya Ukanda wa Gaza ni sehemu ya sera za Marekani na kushiriki nchi hiyo katika jinai dhidi ya watu wa Palestina na kusisitiza kuwa: "Miradi hiyo haina thamani yoyote, na kitu ambacho utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa kukipata kwa kutumia nguvu na mabavu hauwezi kukipata kwa michezo ya kisiasa."

Mojawapo ya malengo ya muda mrefu ya Israel na waungaji mkono wake, akiwemo Donald Trump, ni kufuta kabisa suala la wakimbizi wa Kipalestina katika mlingano wa kisiasa. Suala hili limeibuliwa kwa uzito zaidi na katika sura mbalimbali katika mwaka uliopita sambamba na vita vya Gaza.

Suala la kuwahamisha Wapalestina wanaoishi Gaza na kuwapeleka Libya ni mpango mpya unaopaswa kupewa mazingatia. Mojawapo ya vipengele muhimu vya mpango huo ni kuchagua nchi ya Libya, ambayo haijawa na muundo thabiti wa kisiasa kwa zaidi ya muongo mmoja, kwa ajili ya kuwapa makazi Wapalestina wa Gaza. Baada ya kupinduliwa Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya ilitumbukia katika machafuko na ukosefu wa usalama, na tangu wakati huo haijawahi kuwa na serikali kuu. Makundi tofauti ya wanamgambo na harakati za kisiasa zinadhibiti maeneo mbalimbali ya nchi, na Libya haijawahi kuushuhudia amani na utulivu baada ya zaidi ya miaka kumi ya machafuko ya ndani.

Inaonekana kuwa, katika mazingira hayo, kupewa makazi Wapalestina katika nchi hiyo hakutakabiliwa na upinzani mkubwa wala kuwa na athari mbaya za kimataifa kwa Washington na washirika wake.

Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa kifedha, serikali ya Marekani imeahidi kutoa fedha zinazozuiliwa nchini humo iwapo Libya itakubali kutekeleza mpango huo. Pesa hizo zilikamatwa na kuzuiwa ndani ya mfumo wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa baada ya kuanguka kwa serikali ya Gaddafi, na kuachiliwa na kufika kwa Walibya rasilimali hizi ni muhimu sana kwa watu wa nchi hiyo. 

Kwa kutumia wenzo wa kifedha, Marekani inajaribu kuunda makubaliano ambayo, mkabala wa "kuwapa makazi" Wapalestina, serikali ya Libya au makundi yenye ushawishi ndani ya nchi ndiyo yatakayopokea pesa hizo, ikiwa aina ya biashara ya kisiasa ambayo inaweza hata kuzidisha migawanyiko ya ndani nchini Libya.

Kwa upande mwingine, kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza hadi nchi ya mbali kama Libya, kwa hakika ni hatua ya kuwezesha udhibiti kamili wa Israel juu ya Ukanda wa Gaza. Iwapo idadi ya watu wa Gaza itapungua, suala hilo litafungua njia kwa ajili ya miradi zaidi ya uvamizi ya Israel katika ardhi ya Palestina. Vilevile, kuhamishwa sehemu kubwa ya wakazi wa Gaza, ambayo ni rasilimali-watu ya Muqawama na mapambano ya ukombozi, kutaondoa kikwazo hicho mbele ya Israel, na utawala huo ghasibu utaweza kuwa na udhibiti mkubwa zaidi katika eneo hilo la Palestina kwa msaada wa Marekani.

Tunasisitiza kuwa, mpango mpya wa kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu na kuwapeleka Libya kwa mara nyingine tena unaonyesha kwamba utawala wa Trump na washirika wake bado wanaendelea kukanyaga na kupuuza "haki ya kurejea wakimbizi wa Palestina katika ardhi na nchi yao" kanuni ambayo ni moja ya misingi mikuu ya mapambano ya Wapalestina na imesisitizwa pia katika azimio nambari 194 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha