Araghchi ametoa kauli hiyo kufuatia kumalizika kwa duru ya tano ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington, yaliyodumu kwa zaidi ya saa tatu katika mji mkuu wa Italia, Rome, siku ya Ijumaa. Mazungumzo hayo yalisimamiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi.
Mjumbe huyo mkuu wa Iran katika mazungumzo hayo amesema: “Duru hii ilikuwa miongoni mwa duru za mazungumzo ya kitaalamu zaidi tuliyowahi kushiriki. Tumeweza tena kuweka bayana misimamo na misingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mazungumzo haya. Msimamo wetu uko wazi kabisa, na tutaendelea kuushikilia kwa uthabiti.”
Araghchi ameongeza kuwa upande wa Marekani sasa una “uelewa bora, wa wazi na sahihi zaidi kuhusu misimamo yetu.”
Kabla ya kuelekea Rome, Araghchi alisisitiza azma ya Iran kuendeleza mpango wake wa kurutubisha madini ya urani, akibainisha kuwa hakutakuwa na makubaliano yoyote iwapo Marekani itasisitiza kuondoa kabisa haki halali ya Iran ya kurutubisha urani ndani ya nchi.
Baada ya duru ya tano, Araghchi amesema pande zote mbili zimekubaliana kuwasilisha mapendekezo na mawazo yaliyobadilishanwa wakati wa mazungumzo kwa miji mikuu yao kwa mashauriano zaidi.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran amesema mwenzake wa Oman, kama mpatanishi, alifanya jitihada za kuibua njia za kuondoa vizingiti vilivyopo na kuleta mafanikio.
Amesema Iran inapanga kuchunguza mapendekezo mapya na masuluhisho yaliyowasilishwa, ambayo huenda yakawa na manufaa, huku ikidumisha misimamo na misingi yake.
Araghchi ameelezea matumaini kuwa pande zote zitashiriki mazungumzo ya kina zaidi katika duru ijayo endapo mapendekezo hayo yatazingatiwa na kupokelewa vizuri katika miji mikuu.
Amesema mazungumzo haya ni “magumu zaidi” na masuala yaliyopo hayawezi kutatuliwa katika vikao viwili au vitatu tu, “lakini ukweli kwamba tupo kwenye mwelekeo unaoeleweka ni hatua chanya.”
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Iran ameeleza matumaini kuwa pande husika zitafikia suluhisho litakaloleta mafanikio katika duru zijazo, hasa kutokana na uelewa ulioimarika wa misimamo ya Tehran.
Kama ilivyokuwa katika duru zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani, Donald Trump, katika eneo, Steve Witkoff, waliongoza timu za mazungumzo mjini Rome.
Tangu mwezi Aprili, Tehran na Washington zimefanya duru nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Rome na Muscat kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, huku Marekani ikibadili misimamo mara kwa mara, jambo ambalo limeifanya Iran kuikosoa kwa kile ilichokiita kauli “zinazokinzana” kutoka upande wa Marekani.
Your Comment