Mabadiliko haya ya kimkakati yalitangazwa wazi wakati wa kufanyika luteka ya African Lion, yaani Simba wa Afrika, ambayo ni mazoezi makubwa zaidi ya kijeshi ya pamoja kati ya Marekani na nchi za Afrika. Akizungumza wakati wa kufanyika luteka hiyo, Jenerali Michael Langley, kamanda mkuu wa kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM, alisisitiza haja ya nchi za Kiafrika kufanya "operesheni huru" na "kugawana gharama."
Hata hivyo, Langley amesema Marekani itaendelea kudumisha baadhi ya shughuli za kubadilishana habari za kijasusi na serikali za kijeshi katika eneo la Sahel barani Afrika na pia kwamba inatafuta "njia nyingine za kuendelea kushirikiana na nchi za eneo hilo." Jenerali huyo wa Marekani pia amesema kwamba licha ya kuongezeka hasira huko Washington kuhusu kuimarishwa mahusiano ya Nairobi na Beijing, lakini Kenya itasalia kuwa mshirika wa kimkakati na "mshirika mkuu asiye wa NATO" kwa Marekani.
Mabadiliko haya ya kimkakati yanafanyika katika hali ambayo jeshi la Marekani linasemekana kuchukua hatua za eti "kujenga kikosi kidogo, chenye kasi lakini hatari zaidi," ambazo zinaweza kujumuisha kupunguzwa nafasi za uongozi wa kijeshi katika maeneo kama vile Afrika, huku wapinzani wawili wakuu wa Marekani duniani, yaani China na Russia, wakiendelea kupanua ushawishi wao barani humo. Katika uwanja huo, China imeanzisha mipango muhimu ya mafunzo ya kijeshi kwa majeshi ya Afrika. Russia nayo imepanua uwepo wake barani humo kupitia hatua za usalama na kijeshi, ambapo wakandarasi wake wa kijeshi, hasa Kundi la Wagner, wanaimarisha nafasi zao za kiusalama kote kaskazini, magharibi na katikati mwa Afrika.
AFRICOM ni mojawapo ya matawi kumi ya Jeshi la Marekani katika pembe tofauti za dunia, lililoanzishwa Oktoba 2007 na ambalo lina makao makuu yake huko Stuttgart, Ujerumani. Inasimamia operesheni za kijeshi za Marekani, ikiwa ni pamoja na kushughulikia changamoto na migogoro ya kikanda na kudumisha uhusiano wa kijeshi na nchi 53 za Afrika, isipokuwa Misri, ambayo inasimamiwa na CENTCOM. Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani aliongeza idadi ya kambi za kijeshi za AFRICOM kutoka 3 hadi 84, na hivyo kuongeza barani humo ushindani wa kijeshi wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kama vile Ufaransa. AFRICOM inasimamia takriban askari 9,000 wa jeshi la Marekani barani Afrika.
Hata hivyo, moja ya sera za kijeshi za Rais Donald Trump ni kupunguza uwepo wa jeshi la nchi hiyo katika maeneo mengine ya dunia kwa lengo la kupunguza gharama na pia kukabidhi usalama kwa serikali za kieneo. Kuhusiana na hili, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti mwezi Machi mwaka huu kwamba utawala wa Trump ulikuwa unafikiria kuunganisha Kamandi ya Afrika AFRICOM na Kamandi ya Umoja wa Ulaya ya Marekani EUROCOM kwa lengo la kupunguza muundo na gharama.
Admeli Robert Mueller, mwanzilishi wa AFRICOM, amekiri kwamba moja ya malengo ya kikosi hicho ni "kulinda mtiririko huru wa maliasili kutoka Afrika hadi soko la kimataifa." Hii ina maana kwamba Marekani inapinga serikali za kizalendo zinazopinga tawala za Magharini barani Afrika, unyonyaji na uporaji wa utajiri wa nchi za bara la Afrika, suala linalothibitisha wazi siasa za utawala wa Washington za kuendelea kutoa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kuunga mkono na kuzibakisha madarakani serikali vibaraka na tegemezi katika bara hilo.
Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika zimetumia miaka mingi kupinga kuanzishwa kwa vituo vya kijeshi vya Marekani na mataifa mengine ya kigeni barani Afrika na kuunda vikosi vyao vya pamoja vya kijeshi na mifumo ya usalama. Hatua hizi zinalenga kuzuia kurejea barani humo wakoloni wa Magharibi kwa sura tofauti na visingizio vipya, kama vile eti kudumisha usalama wa nchi za Kiafrika na kupambana na ugaidi. Kupanuka kwa uhusiano wa nchi za Kiafrika na China, nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, pamoja na Russia, hasimu mwingine wa Marekani, kumepelekea kuongezeka kwa uwepo wa nchi hizi mbili barani Afrika, na hili limekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza uwepo na ushawishi wa kijeshi wa nchi za Magharibi, hususan Marekani, katika bara hilo.
Kabla ya 2008, shughuli za kijeshi za Marekani katika bara la Afrika ziliratibiwa na kuendeshwa kupitia vituo vya kijeshi katika maeneo mengine ya dunia. Kuanzishwa kwa AFRICOM kulionyesha kuongezeka kwa maslahi ya usalama ya Marekani katika bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na ushindani wa China na Russia. Hii ni katika hali ambayo ushawishi wa usalama wa Marekani umepungua katika eneo la Afrika Magharibi kufuatia mapinduzi kadhaa ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Serikali ya kijeshi ya Niger mwaka jana iliiamuru Marekani iondoe nchini humo askari wake takriban 1,000 pamoja na kuvunja kambi yake ya ndege zisizo na rubani zenye thamani ya dola milioni 100.
Kwa ujumla, kushindwa kukabiliana na ushindani na ushawishi wa nchi kama vile China na Russia, kubadilishwa vipaumbele vya usalama vya Marekani kuelekea maeneo kama vile Ulaya Mashariki na eneo la Indo-Pasifiki, ukosoaji dhidi ya bajeti kubwa na ya muda mrefu ya kijeshi ya Marekani barani Afrika bila kuwa na matokeo yoyote maalumu na hatimaye upinzani wa nchi za Kiafrika dhidi ya uwepo wa jeshi la Marekani barani humo, yote hayo ni mambo ambayo yamepelekea kubadilishwa mkakati wa kijeshi wa Marekani barani Afrika.
342/
Your Comment