Harvard, chuo kikuu kikongwe na chenye hadhi kubwa zaidi nchini Marekani, hakitaruhusiwa tena kupokea wanafunzi wapya wa kigeni kuanzia Alhamisi, Mei 22. Wanachuo wa sasa pia watalazimika kuhamishiwa kwenye taasisi nyingine za elimu au kuhama kabisa Marekani.
Katika taarifa rasmi, Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani imeituhumu Harvard kwa "kuandaa mazingira ya kuendeleza vurugu na chuki dhidi ya Mayahudi, na kushirikiana na Chama cha Kikomunisti cha China," lakini kinachokosekana katika madai haya yasiyo na msingi ni kuwasilishwa uthibitisho au ushahidi wowote wa kuaminika katika uwanja huo.
Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa uamuzi huu hautokani na masuala ya kiusalama, bali ni jibu la wazi kwa maandamano makubwa ya wanafunzi ya kuunga mkono Palestina na kupinga vita vya Gaza, maandamano ambayo yamevikumba vyuo vikuu mashuhuri vya Marekani kwa wiki kadhaa sasa.
Katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma, Christie Noem, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani ametoa muda wa saa 72 kwa Chuo Kikuu cha Harvard kutoa orodha kamili na taarifa kuhusu wanafunzi wa kigeni hasa wale walioshiriki katika maandamano ya kupinga vita vya jinai huko Gaza. Vinginevyo, kibali cha usajili wa wanachuo wa kigeni kitabatilishwa kabisa.
Makataa haya ya aibu na kusikitisha yanaakisi sera mpya ya utawala wa Rais Trump wa Marekani inayoitwa "Catch and Revoke" ambao ni mpango wa kutambua na kuwafukuza wanafunzi ambao hawakubaliani na mitazamo ya White House.
Tangu kuanza kwa muhula wa pili wa Rais Trump mnamo Januari mwaka huu, mazingira ya masomo nchini Marekani yamekuwa yakikabiliwa na mashinikizo makubwa, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu pekee, visa zaidi ya 1,200 za wanafunzi zimefutwa kwa sababu za kisiasa.
Chuo Kikuu cha Harvard kimesajili zaidi ya wanafunzi 6,800 wa kigeni mwaka huu wa masomo, wakichukua asilimia 27 ya idadi ya wanachuo wote wa chuo hicho.
Raia wa China ndio wanaounda kundi kubwa zaidi, lenye wanafunzi zaidi ya elfu moja; wakifuatiwa na wa Canada, India, Korea Kusini, Ujerumani, Uingereza na Japan. Harvard sio chuo kikuu pekee kinacholengwa na siasa hizo za chuki za serikali ya Trump dhidi ya wageni.
Utawala wa Trump umetishia kufuta msamaha wa ushuru wa vyuo vikuu na hivyo kufuta zaidi ya dola bilioni 2 za ufadhili wa serikali kuu kwa vyuo hivyo. Ikiwa hatua hiyo itatekelezwa, bila shaka itatoa pigo kubwa la kihistoria kwa uhuru wa vyuo vikuu vya kibinafsi.
Awali, vyuo vikuu kama vile Columbia, Princeton na Northwestern pia vimekuwa chini ya mashinikizo sawa na hayo kwa kuunga mkono maandamano ya Wapalestina.
Ikiwa ni katika kujibu hatua hii, Alan Garber, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Harvard ameuita uamuzi huo katika taarifa rasmi kuwa "haramu" na "ukiukaji wa wazi wa uhuru wa kitaaluma" .
Garber amesisitiza kuwa: "Hakuna serikali yoyote, bila kujali misimamo yake ya kisiasa, inayoruhusiwa kuamua vyuo vikuu vya kibinafsi vifundishe nini, viajiri au kumkubali nani, wala kuviainishia maeneo ya kufanya utafiti." Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini Marekani (AAUP) pia kimeonya kwamba serikali "inajaribu kuvitwisha vyuo vikuu mazingira ya kimahakama" ambapo imegeuza uhuru wa taasisi za kitaaluma kuwa uwanja wa vita vya kiitikadi.
Radiamali kuhusu uamuzi huu wa kisiasa haijatolewa nchini Marekani pekee. Muungano wa Vyuo Vikuu vya Ulaya umeliita jambo hilo kuwa "pigo kwa imani ya kimataifa kuhusu elimu ya juu Marekani" na kupendekeza kuwa vyuo vikuu vya Ulaya vijitayarishe kuwakaribisha wanafunzi walioathirika.
Serikali za Ujerumani na Canada pia zimetangaza kuwa zitawezesha mchakato wa kuhamishwa wanafunzi wa kigeni kutoka Marekani.
Taasisi ya Sera za Kimkakati ya Australia imesema kwamba "hii ni fursa ya karne kwa ajili ya kuvutia bongo ambazo zimefukuzwa kutoka Marekani." Pia kumekuwa na hisia kama hizo kutoka Asia Mashariki.
Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Hong Kong kimetangaza rasmi kwamba kitawakubali kikamilifu wanafunzi wa Harvard katika ngazi yoyote ile. Serikali za majimbo nchini China na Hong Kong pia zimeanzisha ofisi maalumu za kuratibu na kuwapokea wanafunzi waliofukuzwa Marekani.
Uchunguzi wa karibuni wa jarida maarufu la Nature umegundua kuwa watafiti watatu kati ya wanne wenye shahada ya uzamivu au juu ya uzamivu wako tayari kuhama Marekani kutokana na sera kandamizi za utawala wa Trump.
Ikiwa hali hii itaendelea, sio tu vyuo vikuu vya Marekani, bali nguvukazi nzima laini ya kitaaluma ya nchi hii itakabiliwa na changamoto kubwa.
Wakati huo huo, Annemarie Slater, mkuu wa taasisi ya wasomi ya New America, ameandika katika uchanganuzi mkali akisema: "Utawala wa Trump unaona vyuo vikuu kama maadui wa ndani hivyo unajaribu kugeuza uhuru wa vyuo vikuu kuwa chombo cha kisiasa."
Huenda hajatia chumvi maneno yake, kwa sababu kinachoendelea huko Harvard leo sio mzozo wa kiidara wala uhamiaji, bali ni mabadiliko makubwa kuhusu maana halisi ya uhuru, kujitawala kitaasisi na mipaka ya uhalali katika demokrasia ya Marekani.
342/
Your Comment