Operesheni hiyo ya kupinga Israel ilifanyika leo asubuhi, ambapo vyombo vya habari vya utawala huo vilithibitisha kwamba safari za ndege katika uwanja wa Ben Gurion zilisitishwa baada ya kombora kurushwa kutoka Yemen.
Gazeti la kila siku la lugha ya Kiebrania, Yedioth Ahronoth, liliripoti kuwa ndege kadhaa zilikwama angani kutokana na kombora hilo kutoka Yemen, likisisitiza kuwa: “Ndege nne zilichelewa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion,” na zilikuwa zikizunguka tu angani.
Jeshi la Israel linaloendeleza ukaliaji wa mabavu katika ardhi za Palestina lilidai kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa ikijaribu kuzuia kombora lililorushwa kutoka Yemen, baada ya kombora la masafa marefu kutambuliwa likielekea kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu.
Vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel pia viliripoti kuwa ving’ora vya mashambulizi ya anga vilisikika magharibi mwa mji wa al-Quds unaokaliwa kwa mabavu, kutokana na hatari ya kombora la balistiki kutoka Yemen.
Jeshi la Yemen limekuwa lilitekeleza mfululizo wa mashambulizi dhidi ya ngome za utawala haramu wa Israel na kuusababishia utawala huo hasara kubwa za kijeshi na kiuchumi.
Opereshenei hizo za kishujaa za vikosi vya ulinzi vya Yemen zinafanywa kwa nia ya kuendelea kukabiliana na mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza. Jeshi la Yemen limesisitiza kuwa litaendeleza mashambulizi yake dhidi ya Israel hadi utawala huo utakapositisha jinai zake dhidi ya Wapalestina.
Your Comment