Akizungumza Jumapili usiku katika hafla ya kuadhimisha miaka 62 ya Umoja wa Afrika mjini Tehran, Waziri Araghchi amelisifu bara la Afrika kwa historia yake ya kupinga ukoloni na kusisitiza mshikamano wa muda mrefu uliopo kati ya Iran na bara hili.
Hafla hiyo, iliyobeba kaulimbiu ya “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia,” ilihudhuriwa na mabalozi kadhaa wa nchi za Afrika pamoja na Waafrika walioko Tehran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Iran na Afrika, Iran inatafuta ushirikiano wa kiuchumi ndani ya mfumo wa AfCFTA na kupitia ushirikiano wa nchi na nchi, kwa imani kuwa Iran na mataifa ya Afrika yanaweza kukamilishana katika nyanja hii na kuimarisha uhusiano wao wa karne nyingi.
Waziri huyo ameeleza kuwa wingi wa rasilimali asilia barani Afrika pamoja na uwezo wa Iran katika teknolojia ya kisasa vinatoa jibu muafaka kwa mahitaji ya pande zote mbili. Amesema kuwa kufanikiwa kwa duru ya tatu ya Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Afrika lililofanyika mwezi uliopita ambalo liliungwa mkono kwa dhati na viongozi wa ngazi za juu wa Afrika, ni ishara njema ya mustakabali wa kupanua ushirikiano baina ya pande hizi mbili, ambao utazidi kuimarika kupitia mikutano ijayo.
Hali kadhalika Araghchi amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa bega kwa bega na Afrika kama rafiki wa kweli wa muda mrefu. Amesema: “Sasa, zaidi ya nusu karne tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizi mbili, tunapaswa kuchukua hatua stahiki kuhakikisha uhusiano huu unadumu." Ameongeza kuwa: "Muungano wa Kusini mwa Dunia (Global South), kwa kuzindua mpango mpya na utaratibu mpya, unaonesha hatima ya pamoja na udugu katika njia ya maendeleo na ustawi.”
Amsisitiza kuwa, kwa fahari na kwa kutambua urafiki huu wa muda mrefu wa kibinadamu, Iran iko tayari kushirikiana na mataifa rafiki ya Afrika katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na siasa, uchumi, viwanda vidogo na vya kati, madini na miundombinu, kubadilishana wahadhiri na wanafunzi, mafanikio ya kisayansi, mafunzo ya rasilimali watu, utalii wa afya, huduma na vifaa vya matibabu, kilimo, mitandao ya umwagiliaji, ujenzi wa mabwawa na sekta nyinginezo.
342/
Your Comment