26 Mei 2025 - 23:22
Source: Parstoday
Araghchi "Ufaransa Haina Mamlaka ya Kimaadili ya Kuihubiria Iran"

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amelaani vikali matamshi ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, aliyoyataja kuwa ya chuki dhidi ya Iran.

Akizungumza Jumapili, Araghchi amesema kuwa maafisa wa serikali ya Ufaransa “hawana mamlaka yoyote ya kimaadili” ya kuihubiria Iran kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Akiikosoa Ufaransa kwa rekodi yake ya ukiukaji wa haki za binadamu, Araghchi amesema kuwa ukiukaji huo umedhoofisha uhalali wa Ufaransa kujiona kama mtetezi wa haki za binadamu duniani.

Ameongeza kuwa: “Msimamo wa Ufaransa kuhusu Israel na uhalifu wa kivita unaofanyika dhidi ya Wapalestina ni mfano wa wazi wa unafiki huu."

Kauli ya Araghchi imekuja baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kumwita kaimu balozi wa Ufaransa (chargé d'affaires) mjini Tehran kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko rasmi kufuatia matamshi ya Barrot yaliyotolewa mapema Jumapili.

Madai hayo yameibuka baada ya filamu ya Muirani, It Was Just an Accident, kushinda tuzo ya Palme d’Or kwenye Tamasha la Filamu la Cannes, ambapo Barrot alielezea ushindi huo kuwa ni ishara ya upinzani dhidi ya ukandamizaji.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imelaani kile ilichokiita ni “utumiaji wa kisiasa wa tukio la kitamaduni” na serikali ya Ufaransa, ikisema Ufaransa imejaribu kutumia tamasha hilo kama jukwaa la kisiasa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter), Waziri Barrot alidai kuwa eti  filamu hiyo “itamsha upya matumaini kwa wapigania uhuru duniani kote” , kauli ambayo ni kuingilia wazi masuala ya ndani ya Iran.

Ufaransa inakabiliwa na tatizo kubwa katika nyanja ya haki za binadamu, ukiwemo ubaguzi wa kimfumo na ubaguzi wa kidini, hasa dhidi ya wahamiaji kutoka Afrika na jamii ya Waislamu.

Matukio ya ukatili wa polisi, vikwazo vya kupita kiasi dhidi ya maandamano ya amani, na vizuizi vinavyowakabili wahamiaji ni miongoni mwa wasiwasi mkubwa unaoendelea kuibuliwa.

Aidha, kuna ukiukaji mkubwa wa  uhuru wa kujieleza ambapo watu wanaounga mkono Palestina na kupinga jinai za Israel wanakandamizwa vikali.

Your Comment

You are replying to: .
captcha