Akizungumza Jumanne mchana kabla ya kuondoka Tehran kuelekea Muscat, Dkt. Pezeshkian amebainisha kuwa ziara hii inafanyika kwa mwaliko rasmi wa ndugu yake, Mheshimiwa Sultan Haitham bin Tariq, na inalenga kutekeleza sera kuu za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi pamoja na juhudi zilizokwisha fanyika katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza uhusiano wa kirafiki na majirani.
Rais amesisitiza kuwa serikali ya kumi na nne imeweka azma ya kuwa na mahusiano bora na mataifa jirani katika nyanja zote zinazowezekana, ikiwa ni pamoja na sekta za kielimu, kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kibiashara. Aidha, amesema kuwa ajenda ya ziara hii inajumuisha pia mazungumzo kuhusu masuala ya amani na utulivu wa kikanda, hali ya Gaza, na kufikia mtazamo wa pamoja katika masuala haya muhimu.
Dkt. Pezeshkian ameongeza kuwa mataifa ya eneo hili yanapaswa kushikamana na kushirikiana ili kusimamisha jinai ambazo hakuna mtu mwenye akili timamu au dhamira ya haki anaweza kuzivumilia. Amesema kuwa hatua hizi ni lazima zipelekwe mbele ya jumuiya za kimataifa kwa msimamo thabiti.
Akizungumzia uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Oman, Rais amesema kuwa thamani ya sasa ya biashara kati ya nchi hizi mbili imefikia takriban dola bilioni 2.3 na inaendelea kuongezeka kwa kasi. Amesema kuwa katika ziara hii, atafanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Oman ili kufuatilia maeneo mbalimbali ya ushirikiano, yakiwemo miundombinu ya barabara, usafirishaji wa majini, biashara, viwanda, elimu, teknolojia na mawasiliano.
Your Comment