Mbali na kuwa mabadiliko ya kiutawala, Mapinduzi ya Kiislamu yaliwadhihirishia wafuasi wake wengi, tofauti kubwa za kisiasa zilizokuwepo kati ya mfumo huu na mifumo mingine ya kiutawala katika nchi za kibeberu za Magharibi. Walitambua kuwa Uislamu haukupaswa kufanywa kuwa ni ibada za kiroho na kitamaduni tu bali ulipaswa kutoa mfano mbadala wa kisiasa, kitamaduni na kijamii, uliojengeka kwenye misingi ya mafundisho yaliyomo kwenye maandiko yake matakatifu.
Imam Khomeini aliyezaliwa mwaka 1900 katika mji wa Khomeyn, nchini Iran, alikuwa mtu mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, si tu kama mwanazuoni wa kidini bali pia kama kiongozi wa mapinduzi.
Akiwa na umri mdogo, aliwapoteza wazazi wake na kulelewa katika familia ya kidini, ambapo baadaye akawa msomi mwenye bidii katika masomo ya Kiislamu. Kisha aliendeleza masomo yake ya kidini katika mji wa Qom, ambako alisoma masomo tofauti ya kidini, ikiwemo falsafa, na irfani. Ujuzi wake mkubwa wa utamaduni wa Kiislamu ulimuwezesha kukwea haraka ngazi za kidini na kuweza kufikia daraja za Ayatollah na kisha Ayatollah Mkuu.
Imam Khomeini (MA) na suala la Quds Tukufu
Imam Khomeini alipoona ufisadi na ushawishi wa nchi za Magharibi ukienea nchini Iran chini ya utawala wa kifalme wa Shah, hapo ndipo ufahamu na hisia zake za kisiasa zilipoanza kustawi na kupata makali. Mnamo 1963, alipinga vikali utawala wa Shah kutokana na mambo mengi mabaya aliyoyaona kikiwemo kile alichokiona kuwa ni uvamizi wa wageni dhidi ya mfumo wa maisha wa Kiirani na Kiislamu. Kwa kufanya hivyo, alikamatwa na baadaye kubaidishiwa katika nchini za Uturuki, Iraq na hatimaye, Ufaransa. Akiwa uhamishoni, aliwaongoza watu wa Iran kupitia hotuba, barua na jumbe zake zilizorekodiwa, katika harakati za mapambano dhidi ya madhalimu.
Baada ya mapigano ya muda mrefu, mwaka 1979 Imam Khomeini hatimaye alifanikiwa kuandaa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, ambayo yalipelekea kupinduliwa kwa Shah na kuasisiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kama Kiongozi Mkuu, alitanguliza na kushajiisha siasa za kupigania haki, uhuru na mshikamano miongoni mwa Waislamu. Pia alikuwa mtetezi mkuu wa wanyonge na akipinga sana ubeberu wa Marekani na Uzayuni.
Imam Khomeini aliaga dunia na kuelekea mbele za Muumba wake tarehe 3 Juni, 1989, lakini fikra zake zingali zipo hai si nchini Iran pekee bali katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na mataifa mengine duniani. Watu wanamthamini sio tu kama mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu bali pia kama mtu aliyetoa msukumo na kuleta sura mpya katika fikra za Kiislamu katika ulimwengu wa sasa. Hata baada ya kifo chake, mfumo aliouanzisha, na maadili aliyoyadumisha ya kupigana dhidi ya ukandamizaji, kujitegemea, na kujitolea kwa ajili ya Uislamu, yangali yanafuatwa kikamili ndani na nje ya Iran na bila shaka jambo hili litaendelea kudumishwa kwa miaka mingi ijayo.
Your Comment