Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa msimu wa Hija ya mwaka huu, ameitaja Hija yenye maarifa na yenye mafundisho ya kina kuwa ni tiba ya maumivu ya sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu.
Akiashiria jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni huko Gaza, Ayatullah Khamenei ameitaja jukumu kuu la serikali za Kiislamu kuwa ni kuzuia kuendelea kwa janga hilo la kibinadamu, na kuiwekea shinikizo Marekani kama mlinzi mkuu wa utawala wa Kizayuni ili isitishe misaada na uungaji mkono wake kwa utawala huo dhalimu. Ameitaka pia mataifa ya Kiislamu kuwa sauti ya kudai utekelezaji wa wajibu huu kutoka kwa tawala zao.
Ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah - 1446 H / 2025 M
“Hija ni Darasa la Maisha ya Tauhidi - Ulimwengu wa Kiislamu Unapaswa Kuchukua Hatua Madhubuti Dhidi ya Jinai za Gaza”
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake wa mwaka huu kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah, ameitaja safari ya Hija kuwa ni mafunzo ya kuhamia kutoka maisha ya kawaida kuelekea maisha ya tauhidi, na amesema:
“Ibada ya Hija imekusanya ndani yake vielelezo vya maisha ya tauhidi, humzoesha Hijaji kwa hakika hiyo na humualika kuitekeleza. Tunapaswa kusikia mwito huo, tujifunze kutokana nao, na tuazimie kuufanyia kazi kwa imani thabiti.”
Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: “Leo hii, ulimwengu wa Kiislamu unayahitaji sana kuliko wakati mwingine wowote mafundisho ya Hija.”
Amebainisha kuwa Hija ya mwaka huu ni msimu wa pili unaofanyika sambamba na jinai mbaya za utawala wa Kizayuni huko Gaza, kisha akauliza kwa kusisitiza:“Ni nani anapaswa kusimama dhidi ya janga hili la kibinadamu?”
Amejibu kwa kusema: “Bila shaka, serikali za Kiislamu ndizo zenye jukumu la kwanza katika suala hili, na mataifa ya Kiislamu yana haki ya kudai kutoka kwao utekelezaji wa jukumu hilo.”
Ayatullah Khamenei ameutaja wazi utawala wa Marekani kuwa ni mshirika kamili wa jinai za Kizayuni huko Gaza, na akaeleza:
“Serikali za Kiislamu zinapaswa kufunga kabisa njia zote za misaada kwa utawala wa Kizayuni, na kuzuia mkono wake katili kuendelea na jinai zake huko Gaza. Washirika wa Marekani katika eneo hili nao wanapaswa kuilazimisha serikali hiyo ya kiimla kusitisha msaada wake kwa utawala huo dhalimu.”
Ameongeza kwa kusema kuwa: “Msimamo wa kishujaa wa wananchi wa Gaza umeifanya Palestina kuwa suala kuu katika fikra za ulimwengu wa Kiislamu na hata kwa wapenda haki kote duniani.”
Na hatimaye akasisitiza:“Ni wajibu wa wasemaji wa umma na watu wenye nafasi katika jamii kuelimisha na kuhamasisha mataifa kuhusu suala la Palestina, kulieneza ombi la kutendewa haki kwa Wapalestina, na mahujaji waliobarikiwa na safari hii watukufu wamuombe Mwenyezi Mungu awape ushindi dhidi ya madhalimu wa Kizayuni na waungaji mkono wao.”
Andiko Kamili la Ujumbe wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah - 1446 H / 2025M
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote. Rehema na amani zimshukie bora ya viumbe, Muhammad Al-Mustafa, Ahlul-Bayt(as) wake watwaharifu, Masahaba wake waliochaguliwa, na wote wanaomfuata kwa wema hadi Siku ya Kiyama.
Hija ni ndoto ya Waumini, ni sikukuu ya wenye shauku, na ni riziki ya kiroho kwa waliobarikiwa. Na ikiwa itafanyika kwa maarifa na kwa kufahamu siri zake za kina, basi bila shaka itakuwa tiba ya matatizo makubwa ya Umma wa Kiislamu, na hata ya ubinadamu wote.
Safari ya Hija si kama safari nyingine za kawaida, kama zile za biashara, utalii au shughuli za kidunia ambazo wakati mwingine huambatana na ibada au matendo ya kheri. Bali, Hija ni mazoezi ya kuhamia kutoka katika maisha ya kawaida kwenda kwenye maisha yanayopendelewa - maisha ya Tauhidi (Umoja wa Mwenyezi Mungu).
Maisha ya tauhidi yanajumuisha mambo kama:
-
1-Kuzunguka daima kuuzunguka mhimili wa haki (Tawafu);
-
2-Kujitahidi daima kati ya miinuko migumu (Sa‘y baina ya Safa na Marwa);
-
3-Kumpiga na kumkataa daima shetani muovu (Ramy al-Jamarat);
-
4-Kusimama kwa unyenyekevu katika dhikri na dua (Arafah na Muzdalifah);
-
5-Kumlisha masikini na wasafiri (Hady na Sadaqa);
-
6-Kuyapuuza tofauti za rangi, kabila, lugha na maeneo ya kijiografia;
-
7-Kuwa mwenye kuwa tayari kuhudumia wengine, kumtegemea Mwenyezi Mungu, na kuiinua bendera ya kutetea haki.
Ibada ya Hija imekusanya vielelezo vyote vya maisha haya ya tauhidi, humzoesha Mwislamu kwa maisha hayo, na humuita ayafuate. Ni wajibu wetu kusikia mwito huo, tujifunze kutokana nao, na tuazimie kwa dhati kuyatekeleza mafunzo ya Hija.
Tunasema tena: Tunapaswa kusikia mwito huu; tufungue mioyo yetu, pamoja na macho ya nje na ya ndani ya nafsi zetu. Lazima tujifunze, na tuazimie kwa dhati kutumia mafunzo haya katika maisha yetu.
Kila mmoja, kwa kadiri ya uwezo wake, anaweza kuchukua hatua katika njia hii – lakini wajibu huu ni mkubwa zaidi kwa wanazuoni, wasomi, viongozi wa kisiasa, na watu wenye nafasi katika jamii.
Ulimwengu wa Kiislamu leo unayahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote mafunzo haya ya Hija. Hii ni Hija ya pili inayoambatana na maafa yanayotokea Gaza na Asia Magharibi. Genge la Kizayuni lenye jinai, linalotawala Palestina, limeifikisha Gaza katika hali ya kutisha kwa ukatili wa kushtusha na uovu usio na kifani.
Sasa hivi watoto wa Palestina wanakufa sio tu kwa mabomu na makombora, bali pia kwa kiu na njaa.
Kila siku idadi ya familia zilizopoteza wapendwa wao – vijana, baba na mama – inaongezeka. Je, ni nani anayepaswa kusimama mbele ya janga hili la kibinadamu?.
Bila shaka, serikali za Kiislamu ndizo wa kwanza kubeba jukumu hili, na mataifa lazima yadhibiti serikali zao na kudai utekelezaji wa wajibu huu.
Ingawa huenda serikali za Kiislamu zikawa na tofauti za kisiasa katika masuala mbalimbali, lakini hali hii haipaswi kuwazuia kushikamana na kushirikiana kuhusu suala la Gaza, ambalo ni mojawapo ya misiba mikubwa zaidi, na kutetea watu waliodhulumiwa zaidi duniani leo hii.
Serikali za Kiislamu zinapaswa kufunga njia zote za misaada kwa utawala wa Kizayuni, na kuuzuia mkono wake katili kuendeleza maovu huko Gaza.
Marekani ni mshirika kamili wa jinai za utawala wa Kizayuni.
Washirika wa Marekani, iwe hapa Mashariki ya Kati au sehemu nyingine za ulimwengu wa Kiislamu, wanapaswa kusikia mwito wa Qur'an wa kuwatetea waliodhulumiwa, na kumlazimisha utawala wa kiimla wa Marekani kusitisha msaada wake kwa utawala huu dhalimu.
Ibada ya Berā’ah (kujiondoa na kuachana na washirikina), katika Hija, ni hatua madhubuti katika mwelekeo huu.
Msimamo wa ajabu wa watu wa Gaza umeuweka tena suala la Palestina katika kilele cha fikra za Ulimwengu wa Kiislamu na wapenda haki kote duniani. Hili ni fursa kubwa inayopaswa kutumiwa kwa haraka, kwa ajili ya kuwasaidia watu hawa wanaodhulumiwa.
Licha ya juhudi za mabeberu na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni za kutaka kufuta jina na kadhia ya Palestina, tabia ya kijinga na maovu ya watawala wa utawala huu, imefanya jina la Palestina kuwa maarufu kuliko wakati mwingine wowote, na chuki ya watu dhidi ya Wazayuni na washirika wao kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kuwa.
Hili ni fursa adhimu kwa Ulimwengu wa Kiislamu
Wasemaji wa jamii na wenye nafasi katika jamii wanapaswa kuwaelimisha watu, kuwahamasisha, na kupanua madai na msimamo kuhusu Palestina. Nanyi, enyi mahujaji waliobarikiwa, msipuuze fursa hii ya dua na kumuomba Mola wenu katika ibada ya Hija, na muombe ushindi dhidi ya wadhulumu wa Kizayuni na waungaji mkono wao.
Rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie Mtume wa Uislamu na familia yake watoharifu, na salamu na baraka zimfikie Imam Mahdi (a.t.f.s) aliyeahidiwa kudhihiri.
Wassalaamu Alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh
Sayyid Ali Khamenei
30 Mei 2025
Your Comment