21 Julai 2026 - 08:26
Walioleta Kambi za Marekani Kuzunguka Iran Leo Wanalia: Kwa Nini Iran Inatushambulia?

Kwa miaka mingi, Iran iliwaonya majirani zake wa Kiarabu kuhusu hatari ya kuruhusu Marekani kujenga kambi za kijeshi katika ardhi zao, ikisema uwepo wa majeshi ya kigeni ungeweza kuzifanya nchi hizo kuwa sehemu ya vita dhidi ya Iran. Leo, baada ya kuanza kwa mapambano, kambi hizo zimegeuka kuwa maeneo ya mashambulizi, huku watawala wa Kiarabu wakijikuta wakikabiliwa na matokeo ya maamuzi waliyoyafanya hapo awali.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Walileta kambi zao za kijeshi katika nchi za Kiarabu ili kuizingira Iran, wakiamini kwamba miaka ya mbele -leo hii- wangetumia kambi hizo kuishambulia Iran kwa msaada wa tawala hizi za Kiarabu.

Kwa miaka yote, Iran haikuwa na wasiwasi na uwepo wa kambi hizo. Iliwaacha Wamarekani wakusanye kambi zao za kijeshi katika nchi jirani na Iran, huku ikijua ni moto gani ambao Wamarekani walikuwa wanauandaa kwa mikono yao wenyewe.

Uwepo wa kambi za kijeshi za Marekani katika nchi zinazoizunguka Iran uliwafanya watawala wa nchi hizo waamini kwamba Marekani ilikuwa katika ardhi zao ili kuwapa usalama na amani.

Iran, kwa miaka yote, ilikuwa ikiwaonya na kuwashauri majirani zake kwamba amani na usalama wao hauwezi kulindwa na taifa la kigeni lililokuja kutoka maelfu ya kilomita mbali. Badala yake, uwepo wa adui huyo katika ardhi zao ungeweza kuwa hatari kwao, hasa iwapo adui huyo angeitumia ardhi yao kuishambulia Iran.

Iran iliwaambia wazi kwamba siku ambayo Marekani itaitumia ardhi yao kama msingi wa mashambulizi dhidi ya Iran, nchi hizo zingeweza kujikuta zikiwa sehemu ya mapambano ambayo hawakuyataka.

Lakini hawakuelewa nasaha hizo za Iran kwa wakati huo. Waliamini kwamba Marekani ndiyo “mungu mtu” wao; kwamba imekuja kuwalinda dhidi ya hatari ya Iran. Wakaamini ahadi hizo na wakadanganyika.

MWAKA 2026: VITA ILIANZA, NA KILICHOFICHWA KIKAFICHUKA

Mwaka huu wa 2026, vita ya adui ilipoanza dhidi ya Iran, Iran ikajibu kwa nguvu kubwa. Kambi za kijeshi za Marekani zilizokuwa katika nchi jirani za Kiarabu zikaanza kukabiliwa na mashambulizi makali ya Iran.

Wamarekani wakaanza kutafuta maeneo ya kukimbilia na kujificha kutokana na moto 🔥 wa makombora ya balistiki ya Iran.

Hapo ndipo Waarabu wakaanza kushangaa. Wakajikuta kwamba kumbe wao ndiyo waliobeba jukumu la kuwahifadhi, kuwahami na kuwaokoa wanajeshi wa Marekani kutokana na moto wa Iran wenye ghadhabu.

Wanajeshi wa Marekani wakaanza kuyakimbia makambi yao ya kijeshi na kukimbilia katika hoteli na maeneo mengine waliyoamini kuwa yangekuwa salama zaidi.

Lakini Iran haikuwa ikipigana kwa kubahatisha. Ilipata taarifa za kiintelijensia kuhusu maeneo ambayo wanajeshi hao walikimbilia kujificha, na maeneo hayo yakawa pia sehemu ya mashambulizi.

Hapo ndipo watawala wa Kiarabu wakaanza kulalamika:

“Eeeh! Iran inatushambulia!”

“Marekani haikulinda sisi!”

“Kwa nini tunalazimika sisi kuwalinda na kuwahifadhi wanajeshi wa Marekani?”

Lakini swali la msingi ni hili:

Mlipowaruhusu Wamarekani kujenga kambi za kijeshi katika ardhi zenu, mkawawezesha kuzitumia kama vituo vya kijeshi dhidi ya Iran, mlidhani nini kingetokea siku ambayo vita ingeanza?

Iran ilikuwa imewaonya tangu mwanzo.

Iliwaambia kwamba taifa la kigeni lililokuja kutoka maelfu ya kilomita mbali halikuwa likija kuwaletea amani ya kweli. Iliwaambia kwamba uwepo wa majeshi ya kigeni katika ardhi zao ungeweza kuwafanya kuwa sehemu ya vita vya wengine.

Lakini walipuuza nasaha hizo.

Leo, walipojenga kambi za Marekani katika nchi zao, hawakubeba tu “ulinzi wa Marekani”; walibeba pia uwezekano wa ardhi zao kuwa sehemu ya mapambano iwapo Marekani ingetumia kambi hizo kuishambulia Iran.

Ndiyo maana Iran haikuwa na haraka ya kuzuia Marekani kujenga kambi hizo.

Iliwaacha wajenge.

Iliwaacha wakusanye silaha.

Iliwaacha waweke ndege zao za kivita.

Iliwaacha waweke makombora na mifumo yao ya kijeshi.

Kwa sababu wakati mwingine, adui anapojikusanya mwenyewe karibu yako, anakuwa amekurahisishia kazi ya kumfikia.

Na leo, kile ambacho kilijengwa kwa madai ya “kuilinda Marekani na kuizingira Iran” kimegeuka kuwa maeneo ambayo Iran inaweza kuyafikia kwa urahisi zaidi wakati wa mapambano.

Qur’ani Tukufu inaelekeza:

“Na waandalieni nguvu kama muwezavyo...”

(Qur’ani, Surah Al-Anfal 8:60)

Ujumbe wa Qur’ani ni kwamba nguvu, maandalizi, tahadhari na uwezo wa kujilinda ni mambo muhimu katika kukabiliana na maadui.

Kwa hiyo, wakati adui anatumia miaka mingi kujiandaa, kujenga vituo, kukusanya silaha na kuzunguka nchi yako, usidanganyike na ukubwa wa kambi zake.

Wakati mwingine, kambi nyingi za adui hazimaanishi kwamba adui yuko salama.

Huenda zikawa ni ramani ya maeneo ambayo adui mwenyewe amekuchorea ili uyafikie wakati wa mapambano.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha