18 Julai 2026 - 16:09
IRGC Yatangaza Operesheni Kubwa za Kujibu Dhidi ya Vituo vya Kijeshi vya Marekani Katika Nchi Sita

Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) wametangaza operesheni za kijeshi za kujibu kile walichokitaja kuwa ni uchokozi wa Marekani, huku vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi kadhaa za eneo hilo vikidaiwa kulengwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) wametangaza rasmi kuanza kwa operesheni za kijeshi za kujibu uchokozi wa Marekani, wakieleza kuwa mashambulizi hayo yaliyofanyika usiku uliopita na leo yalikuwa makubwa na yalisababisha madhara makubwa kwa vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mashambulizi hayo yalilenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika nchi kadhaa, zikiwemo Syria, Jordan, Kuwait, Bahrain, Qatar na Oman.

Taarifa hizo zinadai kuwa katika mashambulizi hayo, rada kadhaa, ndege za kivita zilizokuwa ardhini, helikopta pamoja na mifumo ya kurusha makombora inayodaiwa kutumiwa na Marekani viliharibiwa.

Aidha, kwa mujibu wa madai hayo, baadhi ya vituo vya Marekani nchini Syria vililengwa kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni kuzuia kwa silaha zilizokuwa zikielekea kwa Hizbullah.

Mashambulizi hayo yameelezwa kuwa sehemu ya operesheni za kulipiza kisasi na kujibu hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran, huku hali ya kijeshi katika eneo hilo ikiendelea kuwa ya wasiwasi na mvutano mkubwa.

Ramani ya maeneo yanayodaiwa kulengwa imeandaliwa ili kurahisisha ufuatiliaji wa maeneo yaliyotajwa na kuelewa kwa urahisi wigo wa operesheni hizo.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha