5 Juni 2025 - 15:56
Source: Parstoday
Jeshi la Iran latoa tahadhari: Tuko tayari kukabiliana na "Makosa ya Kimkakati" ya maadui

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesisitiza utayari wake kamili wa kukabiliana na vitendo vyovyote vya uchokozi au makosa ya kimkakati kutoka kwa maadui wa taifa la Iran, kwa wakati wowote na kwa kiwango chochote.

Taarifa hiyo imetolewa na Makao Makuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 36 tangu kuaga dunia kwa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhollah Khomeini.

"Kwa uongozi wake wa kipekee, wa kimiujiza, pamoja na haiba yake ya kihistoria kama msomi mkubwa wa dini na mbunifu wa karne hii, Imam Khomeini alianzisha mfumo wa kiungu uliojengwa juu ya misingi ya demokrasia ya kidini na mafundisho ya Kiislamu. Mfumo huu ulivunja mpangilio wa dunia wa kisasa wa upande wa Magharibi na Mashariki, na kuibua nguvu mpya kama Mapinduzi ya Kiislamu katika medani ya kimataifa," ilisomeka taarifa hiyo.

Jeshi la Iran limebainisha kuwa taifa la Iran, lenye ujasiri, hekima na moyo wa kishujaa, litaendelea kushinda changamoto, vikwazo, mashinikizo, na matatizo yoyote chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

"Jeshi litatawafanya maadui kujutia vitendo vyao kwa kusimama imara dhidi ya vitisho, njama, uchokozi na uovu wa mfumo wa kiulimwengu wa kiunyonyaji, huku wakiendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali za maendeleo na uwezo wa kitaifa."

Taarifa hiyo imesisitiza kuwa “Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vyenye uwezo mkubwa, ujasiri na utayari wa kupigiwa mfano, viko tayari kukabiliana na chokochoko au makosa yoyote ya kimkakati kutoka kwa maadui, kwa kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu na uongozi wa busara wa Amiri Jeshi Mkuu.”

Pia ilieleza kuwa vikosi hivyo ni nguzo kuu ya usalama wa taifa la Iran na vinafuatilia kwa karibu mienendo na mipango ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Tangu Aprili 12, Iran na Marekani zimekuwa zikifanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran unaolenga matumizi ya amani. Pamoja na kuwepo mazungumzo hayo, Marekani imekuwa ikitoa vitisho vitisho vya kijeshi dhidi ya Iran.

Kwa upande mwingine, utawala haramu wa Israel umekuwa ukitishia kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran endapo mazungumzo hayo yanayoendelea baina ya Tehran na Washington chini ya usuluhishi wa Oman yatavunjika.

Mwaka jana, Jamhuri ya Kiislamu ilirusha makombora dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel katika Operesheni "Ahadi ya Kweli I na II", kama jibu kwa shambulio la utawala huo haramu dhidi ya ubalozi wake nchini Syria, pamoja na mauaji ya viongozi waandamizi wa harakati za upinzani za Palestina na Lebanon, na kamanda mwaandamizi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Your Comment

You are replying to: .
captcha