2 Julai 2025 - 13:28
Source: Parstoday
Mataifa yaahidi kusaidiana ili kufikia mwafaka wa mzigo wa madeni

Kongamano la Kimataifa la ufadhili kwa ajili ya maendeleo limemalizika nchini Uhispania kwa taifa hilo kutangaza kupeleka dola bilioni 1.9 katika Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF za kusaidia nchi zinazoendelea.

Akthari ya mataifa 100 yaliyohudhuria kongamano hilo la kimataifa yameahidi kusaidia kupata suluhu ya kile walichokitaja kama "bomu linalosubiri kulipuka" kwa kuzingatia mzigo wa madeni unaozidi kuyaelemea mataifa yanayoendelea, ingawa yakijikuta kwenye mgawanyiko kuhusiana na namna ya kukabiliana na tatizo hilo.

Akihutuubia kongamano hilo, Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba "mzigo wa madeni unaulemaza ulimwengu unaoendelea,"na kusisitiza juu ya kuweko nguvu ya pamoja katika kuyasaidia mataifa hayo yenye kipato cha chini kuondokana na jinamizi hilo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, deni la nje la nchi masikini zaidi limeongezeka zaidi ya mara tatu katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Mataifa yanayoendelea kwa sasa yanalazimika kuwalipa wakopeshaji dola trilioni 1.4 kila mwaka kulingana na masharti ya mkopo, kiwango kilichoongezeka sana katika miaka 20. Mataifa ya masikini pia yanakabiliwa na mzigo wa riba ambao ni mara mbili zaidi ya mataifa tajiri.

Wakati huo huo, Uhispania imeahidi kupeleka nyongeza ya dola bilioni 1.9 katika Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, kama sehemu ya juhudi za kuzisaidia nchi zinazoendelea.

Waziri wa Uchumi Carlos Cuerpo amesema pambizoni mwa kongamano hilo kuwa Uhispania itaendelea kuwa mfano katika mchakato wa kupata suluhu kwa kutoa sehemu ya fedha kwa maslahi ya mataifa yanayoendelea.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha