2 Julai 2025 - 13:30
Source: Parstoday
UN: Israel imekiuka sheria za kimataifa kwa kuwalenga raia wa Iran

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekiuka pakubwa sheria za kimataifa kwa kuwaua shahidi wanafamilia wa wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida wa Iran.

Thameen Al Kheetan, Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, alisisitiza jana Jumanne kwamba kitendo cha utawala wa Israel kuwaua wanafamilia wa wanasayansi wa Iran ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, kwa sababu raia wanapaswa kulindwa.

Al Kheetan amesema: "Raia ni watu ambao si wanachama wa jeshi, na mashambulizi dhidi yao ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu."

Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa wanafamilia kadhaa wa wanasayansi wa nyuklia wa Iran pia wameuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kuongeza kuwa, familia za wanasayansi, sawa na raia wengine, zina haki ya kulindwa.

Katika hujuma yake ya kikatili dhidi ya Iran, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilenga nyumba kadhaa za wanasayansi na makamanda wa jeshi na kuua shahidi watu wengi wa familia zao.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha