Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Dar es Salaam, Tanzania [28-08-2025] - Katika Mnasaba adhimu wa kuwadia kwa Mwezi Mtukufu wa Rabiul Awwal, Mwezi uliobarikiwa na ambao ndani yake alizaliwa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w), Sheikh Mohammed Mubarak, Imam Mkuu Masjid Bilal Udoe - Lumumba Road, Kariakoo, Dar-es-Salaam ametoa salamu maalumu kwa Waislamu wote duniani, ambao ni Wapenzi na Wafuasi wa Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Sheikh Mubarak amesisitiza kwamba Mwezi huu ni fursa ya kipekee kwa Waislamu ulimwenguni kote kuungana kwa sauti moja katika kumtukuza na kumuenzi Mtume wa Rehma, Muhammad (s.a.w.w).
Amesema kuwa nchini Tanzania, waumini wamekuwa wakisherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume (Maulid) kupitia mikusanyiko mbalimbali inayofanyika katika maeneo tofauti, ikiwemo misikiti, viwanja vya wazi na majumba ya ibada.
Kwa mujibu wa Sheikh Mubarak, maandalizi haya na sherehe za Maulid siyo tu kumbukumbu ya kihistoria, bali pia ni nafasi ya kuimarisha mshikamano, mapenzi na mshikikano wa umma wa Kiislamu nchini na duniani kote.
Aidha, amewataka Waislamu kutumia mwezi huu mtukufu kuenzi mafundisho ya Mtume (s.a.w.w), kuyaishi mafunzo yake ya huruma, mshikamano, haki na upendo kwa viumbe wote.
Your Comment