Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Gilgit-Baltistan, Pakistan – Naibu Mwenyekiti wa chama cha Majlis Wahdat-e-Muslimeen Pakistan, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad Iqbal Rizvi, ameonya juu ya hali mbaya inayolikumba eneo la Gilgit-Baltistan, akibainisha kuwa wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na mafuriko ya maangamizi, ukandamizaji wa Serikali, ufisadi na uzembe wa viongozi.
Akizungumza katika taarifa kwa vyombo vya habari, Rizvi alisema:
- Wafanyabiashara katika eneo la mpakani wako kwenye mgomo wa amani kudai haki zao halali, lakini wanakabiliana na ukandamizaji wa serikali, ukatili wa polisi na mbinu za kifashisti.
- Wanasheria, walimu, polisi na watumishi wengine wa umma nao wamemiminika mitaani wakipaza sauti kudai haki zao.
- Hali ya sasa inawafanya wananchi kuhisi kwamba watawala wao ni kama mzigo mzito na adhabu isiyostahimilika.
Aidha, aliongeza kuwa mafuriko yaliyotokea yameharibu mashamba na vijiji, kuyaacha maeneo ya mabonde yaliyokuwa “peponi” yakiwa magofu, huku maelfu ya watu wakibaki bila makazi. Licha ya hayo, serikali ya mitaa na ile ya shirikisho hazijachukua hatua za maana, jambo linaloongeza hasira na kukata tamaa kwa raia.
Kiongozi huyo wa kidini wa Shia Pakistan alisisitiza kuwa leo hii, rushwa, ukosefu wa sheria na usimamizi mbovu ndizo zimeenea kote katika eneo la Gilgit-Baltistan. “Wananchi wanajiona wapo peke yao, wamenyimwa haki na hawana pa kutegemea. Endapo hali hii itaendelea, ghadhabu ya wananchi inaweza kubadilika na kuwa dhoruba kubwa ambayo mzigo wake utabebwa na watawala pekee,” alionya.
Your Comment