11 Oktoba 2025 - 22:15
Source: Parstoday
Iran: Tutalinda maslahi yetu Ghuba ya Uajemi hadi tone la mwisho la damu

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amegusia uwezekano wa kutokea vita vya moja kwa moja vya kijeshi baina ya Iran na Marekani katika Ghuba ya Uajemi na kusema: Tutajihami na kulinda maslahi yetu katika Ghuba ya Uajemi hadi tone la mwisho la damu.

Jenerali Alireza Tangsiri, amesema hayo wakati akizungumzia Muqawama wa Jeshi la Wanamaji la SEPAH dhidi ya uvamizi wa Marekani katika miaka ya huko nyuma na kusisitiza kuwa: Wakati huo, silaha yenye nguvu zaidi tuliyokuwa nayo ilikuwa ni RPG na baadaye tukaweza kupata silaha iitwayo 107. Wakati huo hatukuwa na kinga angani wala hatukuwa na silaha nyingi. Lakini pamoja na hali ngumu sana kama hiyo tulisimama imara kupambana na Marekani katika vita visivyo na mlingano sawa na maadui walishindwa kufikia malengo yao.

Ameongeza kuwa: Ni vyema wananchi wapendwa wa Iran wafahamu kwamba Jeshi la Wanamaji la SEPAH limetoa mashahidi 9 wa kulinda Haram tukufu katika eneo la Ghuba ya Uajemi, wakiongozwa na Shahidi Mahdavi na wanamapambano wenzake shupavu.

Amesema: Kati ya jumla ya vipigo 9 vikubwa ambavyo SEPAH imeipiga Marekani, 6 kati yake vilikuwa ni vya wakati wa vita vya Kujihami Kutakatifu, (vita vya miaka minane ilivyolazimishwa Iran kupigana na utawala wa zamani wa Iraq). 

Jenerali Tangsiri amezungumzia pia Lango Bahari la Hormuz na kusisitiza kuwa, lango hilo ni "mshipa wa uhai wa nishati za mafuta na gesi duniani" na kwamba Iran daima imekuwa ikilinda usalama wa lango hilo.

Amma kuhusu nguvu za makombora za Iran, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la SEPAH amesema kuwa, hivi sasa Iran ni nguvu kubwa ya makombora kwenye eneo hili na iko tayari kuuza makombora na zana zake za kijeshi kwa mataifa mengine duniani. 

Your Comment

You are replying to: .
captcha