10 Oktoba 2025 - 08:38
Kuhusu Kuachiwa kwa Wafungwa Maarufu wa Kipalestina / Hatma ya Mwili wa Shahidi Yahya Sinwar Katika Mkataba wa Kusitisha Mapigano

Sambamba na makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Harakati ya Mapambano ya Kipalestina (Muqawama) na utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza, vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti tetesi na tafsiri tofauti kuhusu masharti ya makubaliano hayo na namna yatakavyotekelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) –ABNA–, Osama Hamdan, mmoja wa viongozi wakuu wa Hamas, katika mahojiano na kituo cha habari cha Al-Arabi alieleza baadhi ya mambo ambayo Hamas inatarajia, pamoja na yale ambayo tayari yamekubaliwa.

Miongoni mwa mambo yanayojadiliwa ni kuachiwa kwa wafungwa wa Kipalestina, jambo ambalo limezua maoni na mijadala mikubwa katika vyombo vya habari.
Kituo cha Al-Arabi cha Qatar kilimnukuu Hamdan akisema kuwa makubaliano yaliyofikiwa “ni mwisho wa vita,” na kwamba Hamas itakabidhi usimamizi wa Ukanda wa Gaza kwa viongozi wa Kipalestina bila kuingiliwa na Israel.

Naye msemaji wa Hamas, akizungumza na Al-Jazeera, alisisitiza kwamba silaha za mapambano ni halali kisheria na kimaadili, kwa kuwa ni ngao ya kujilinda na kuhakikisha uhuru wa maamuzi ya Kipalestina.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wapalestina hawana imani na Israel, wakisema kuwa “mavamizi hayo mara nyingi hayatekelezi makubaliano, hukwepa muda uliopangwa na hufanya ujanja kuhusu orodha ya wafungwa.” Wameitaka jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Israel iheshimu makubaliano hayo.

Hata hivyo, licha ya taarifa kwamba Israel imekubali kuachia Marwan Barghouti (kiongozi wa chama cha Fatah) na Ahmad Sa’adat (kiongozi wa Popular Front), ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imesema wazi kuwa Marwan Barghouti hatakuwa sehemu ya makubaliano hayo.

Gazeti la Kizayuni Jerusalem Post linaripoti kwamba kikosi maalum cha pamoja kati ya Israel, Marekani, Misri, Qatar na Uturuki kimeundwa ndani ya saa 72 ili kushughulikia urejeshaji wa miili na mateka wa pande zote mbili.
Hata hivyo, vyanzo vya Kiebrania vimesema kuwa miili ya Yahya Sinwar na ndugu yake Muhammad haitakabidhiwa kwa upande wa Palestina katika makubaliano hayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye ametaka mateka wote waachiwe huru kwa heshima na kwamba kuwe na kusitishwa kamili kwa mapigano ili kudumisha amani ya kudumu.

Licha ya matangazo ya vyombo vya habari vya Israel kuhusu kuanza kwa usitishaji mapigano, ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo imesema kuwa makubaliano hayajaanza kutekelezwa rasmi, na utekelezaji wake unategemea kikao cha Baraza la Mawaziri la Netanyahu kitakachofanyika leo jioni.
Kituo cha televisheni cha Channel 13 cha Israel kimefafanua kuwa: “Israel kwa sasa haitaanza oparesheni yoyote mpya ya kijeshi, lakini kuondoka kwa majeshi yake Gaza kutategemea uamuzi wa baraza la mawaziri.”

Wakati huohuo, licha ya tangazo la kusitisha mapigano, mizinga ya Israel katika eneo la Netzarim, kusini mwa Gaza, imeripotiwa kufyatua risasi kwa raia waliokuwa wakijaribu kuelekea kaskazini, jambo lililozua taharuki miongoni mwa wakaazi.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha