Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Shule ya Mabanati wa Kiislamu inayoitwa "Madrasat Hazrat Zainab (sa), iliyopo Kigamboni, Dar-es-salaam - Tanzania, ambayo ni sehemu ya Taasisi za Jamiat al-Mustafa (s) - Tanzania, chini ya usimamizi wa Dr.Ali Taqavi, kila Ijumaa asubuhi hufanya Ibada Muhimu ya Usomaji wa Dua Muhimu inayoitwa na kujulikana kama Dua'u al-Nudba. Kwa hakika Dua hii ni Muhimu na ina maana Kubwa mno na baraka Tele kwa mwenye kuizingatia na kuisoma kila wiki (Siku ya Ijumaa). Ufuatao ni Ufafanuzi kuhusu Umuhimu wa Dua ya Nudba.
Dua ya Nudba ni moja kati ya dua zenye maana ya kina na nafasi maalum katika mafundisho ya Kiislamu, hasa katika madhehebu ya Shia. Neno “Nudba” kwa Kiarabu linamaanisha kulia au kuomboleza kwa uchungu na shauku, na dua hii ni nidaa ya upendo na huzuni ya waumini kwa Imam wa Zama – Imam Mahdi (a.t.f.s), ambaye kwa imani ya Waislamu wengi bado yuko hai na yupo katika ghaiba (ukosekanaji wa dhahiri).
Asili na Chanzo cha Dua
Dua hii imeripotiwa kutoka kwa Imam Ja’far Sadiq (a.s) na imehifadhiwa katika vitabu mashuhuri vya dua kama Misbahul Mutahajjid na Iqbalul A’mal. Kwa kawaida, Dua ya Nudba husomwa kila siku ya Ijumaa asubuhi, kwani siku ya Ijumaa inahusishwa moja kwa moja na Imam Mahdi (a.s) – siku ya matumaini ya kudhihiri kwake.
Maudhui Makuu ya Dua ya Nudba
Dua hii inabeba ujumbe mpana wa kiroho na kielimu unaomkumbusha muumini historia ya Mitume na Maimamu (a.s) pamoja na nafasi yao katika kuongoza wanadamu. Maudhui yake muhimu ni pamoja na:
- Kueleza falsafa ya Uimamu na umuhimu wa uongozi wa Kiungu.
- Kukumbuka mateso na dhulma zilizowakumba Ahlul-Bayt (a.s).
- Kuonyesha shauku na hamu ya dhati ya kukutana na Imam Mahdi (a.s).
- Kukuza roho ya matumaini, uaminifu na utayari wa kumnusuru Imam atakapo dhihiri.
Umuhimu wa Kiroho na Kielimu
Kusoma Dua ya Nudba huamsha hisia za mapenzi na uhusiano wa kiroho kati ya muumini na Imam wake, huku ikiondoa hali ya kutojali na kusahaulika. Ni ahadi ya upya ya uaminifu kwa Imam wa zama, na chachu ya kuimarisha imani, subira na msimamo katika njia ya haki.
Kuhusu Utekelezaji wa Dua katika Shule ya Mabinti
ya Hazrat Zainab (sa), Kufanyika kwa Dua ya Nudba kila Ijumaa baada ya Swala ya Asubuhi, kwa ushiriki wa Wanafunzi wote na wasimamizi wao, ni hatua muhimu katika kukuza mazingira ya kiroho, malezi ya kiimani, na kuimarisha utamaduni wa kumkumbuka Imam Mahdi (a.s) kila wiki, na kuomba Dua ya kuharakisha kudhihiri kwake kwa ajili ya kuenea kwa Haki na Uadilifu Duniani.
Ibada hii hujenga umoja wa kiroho, maadili mema na moyo wa subira, na hivyo kufanya wiki kuanza kwa baraka na nuru ya dua.
Your Comment