Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Jana Ijumaa, Tarehe: 10 Oktoba 2025 / 17 Rabiul Thani 1447H.Q, Sala ya Dhuhri ilisaliwa katika Chuo cha Mabinti wa Kiislamu cha Hazrat Zainab (sa), kilichopo Kigamboni - Jijini Dar-es-salaam, iliyoambatana na mada muhimu kuhusiana na umuhimu wa: Taq'wa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kitengo cha utamaduni wa Chuo husika, ibada tukufu ya Sala ya Dhuhri ya Siku ya Ijumaa ilifanyika kwa utaratibu mzuri katika Chuo hicho, ikiudhuriwa na Imam na Khatibu wa Kiroho, Sheikh Dkt. Swaleh Maulid.
Katika ibada hiyo adhimu, Wanafunzi wa Chuo, Masheikh, pamoja na wasimamizi wa Wanafunzi walihudhuria kwa wingi. Sala ilianza kwa wakati uliopangwa na ilidumu kwa takriban dakika 45.
Katika Khutba ya Kwanza, Sheikh Swaleh alisisitiza juu ya umuhimu wa Taq'wa (Uchaji Mungu) kama msingi wa mafanikio ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Alinukuu kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo:
"Enyi Mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na semeni maneno ya sawa (maneno ya Haki)."
(Surat Al-Ahzab, 70).
Akasema kwamba waja wa Allah wanapaswa kuwa wa kweli katika maneno na matendo yao, na kwamba wanafunzi wa dini wanapaswa kuwa kielelezo cha uaminifu, ukweli na ucha Mungu katika jamii.
Katika Khutba ya pili, Sheikh Swaleh aligusia masuala ya kijamii na maadili ya kila siku, akisisitiza umuhimu wa umoja, nidhamu katika ratiba za chuo, na kuheshimiana baina ya wanafunzi na walimu.
Aidha, alitoa shukrani kwa uongozi na wanafunzi waliotoa ushirikiano katika maandalizi na utekelezaji wa ibada hiyo ya Dhuhri (Siku ya Ijumaa) kwa utulivu na nidhamu.
Mwisho wa ibada, Waumini walihitimisha kwa kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kuomba Dua ya faraja na kudhihiri kwa haraka kwa Imam Mahdi (a.t.f.s).
Lengo Kuu la mada iliyowasilishwa ni: Kukuza roho ya ibada, kuimarisha umoja wa kijamii, na kuhimiza utamaduni wa Sala ya Ijumaa miongoni mwa wanafunzi wa dini.
Your Comment