9 Oktoba 2025 - 22:01
Mufti Mkuu Sheikh Dkt. Abubakar Zubair akutana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kujadili kuhusu njia za Kuimarisha Maadili na Ucha Mungu katika Jamii

Ziara hii ya Mufti Mkuu ni miongoni mwa juhudi endelevu za uongozi wa Kiislamu nchini katika kujenga maadili, amani na mshikamano wa kijamii, sambamba na kutoa wito wa kuzingatia uadilifu na uchamungu katika kila nyanja ya maisha.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- 

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuberi bin Ally, amefanya ziara rasmi ya kirafiki na mazungumzo ya kidini na kijamii kwa kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, ofisini kwake mkoani humo.

Mufti Mkuu Sheikh Dkt. Abubakar Zubair akutana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kujadili kuhusu njia za Kuimarisha Maadili na Ucha Mungu katika Jamii

Katika mazungumzo yao, Mufti Dkt. Abubakar alielezea kwa kina juu ya changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili unaoikabili jamii kwa sasa, akisisitiza umuhimu wa viongozi wa dini na serikali kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha misingi ya malezi, maadili na uchamungu miongoni mwa wananchi, hususan vijana.

Amesema kuwa moja ya jukumu kuu la viongozi wa dini ni “kutengeneza nyoyo za waumini”, ili ziwe thabiti katika imani, maadili na utiifu kwa Mwenyezi Mungu, jambo litakalosaidia kupunguza vitendo vya uhalifu, uvunjifu wa amani, na mienendo isiyofaa katika jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, alimshukuru Mufti Mkuu kwa ziara hiyo yenye tija, akieleza kuwa mkoa wa Iringa uko tayari kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) katika mipango na mikakati ya kukuza maadili, elimu ya dini, na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Ziara hii ya Mufti Mkuu ni miongoni mwa juhudi endelevu za uongozi wa Kiislamu nchini katika kujenga maadili, amani na mshikamano wa kijamii, sambamba na kutoa wito wa kuzingatia uadilifu na uchamungu katika kila nyanja ya maisha.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha