11 Oktoba 2025 - 22:18
Source: Parstoday
Kwa nini Trump amekosa Tuzo ya Amani ya Nobel?

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kukosa Tuzo ya Amani ya Nobel, msemaji wa Ikulu ya White House ameikosoa Kamati inayoandaa Tuzo ya Nobel kwa kutomtunuku rais huyo tuzo hiyo, akiitaja hatua hiyo kuwa ni upendeleo wenye kufadhilisha siasa badala ya amani.

Steven Cheung Mkurugenzi wa Mawasiliano wa White House amesema katika taarifa kuwa: "Rais Trump anaendelea kufanya juhudi ili kufikia makubaliano ya amani, kumaliza vita na kuokoa maisha ya watu". Amedai kuwa Trump ana moyo wa kibinadamu na kwamba hakutakuwa na mtu kama yeye ambaye anaweza kufanya hivyo kwa mapenzi na irada yake mwenyewe. Kamati ya Tuzo ya Nobel imethibitisha kuwa inafadhilisha siasa kuliko amani. Radiamali hii kali si tu imedhihirisha kutoridhishwa Washington na uamuzi wa Kamati ya Nobel, bali kwa mara nyingine tena imeibua mijadala mikubwa kuhusu taswira ya kisiasa ya tuzo hiyo na ustahiki halisi waTrump mkabala wa kutunukiwa tuzo hiyo. 

Akiwa rais wa nchi, Trump amejaribu mara kadhaa kujiarifisha kuwa mtu anayependa amani. Hata hivyo vitendo kama kuuliwa kigaidi Kamanda shahidi Qassim Suleiman mwezi Januari 2020 mauaji yaliyolisukuma eneo la Asia Magharibi katika ukingo wa vita, kuifunga njia ya diplomasia kufuatia kuiondoa Marekani kwa upande mmoja katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kuhamishia ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas jambo lililochochea ghadhabu za Ulimwengu wa Kiislamu, na kuunga mkono bila masharti muungano wa Saudia dhidi ya Yemen katika muhula wake wa kwanza wa urais, yote haya yanadhihirisha mwenendo usio na uhusiano wowote na suala la amani. 

Hatua hizi zimeendelezwa pia katika duru ya pili ya urais wa Trump. Kuiunga mkono Israel bila masharti katika vita dhidi ya Gaza, mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Yemen kwa shabaha ya kuuhami utawala wa Kizayuni, kutekeleza mashambulizi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kwa ushirikiano na utawala wa Kizayuni kitendo ambacho ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, uwepo wa  meli za Marekani katika Bahari ya Caribbean kwa kisingizio cha kupambana na magenge ya magendo ya dawa za kulevya, kukabiliana na wahajiri wanaoishi Marekani, na kuwawekea mashinikizo wanafunzi na wanaharakati wa taasisi za kiraia wanaounga mkono kadhia ya Palestina ndani ya Marekani, ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na Donald Trump ambazo si tu hazijaimarisha amani bali zimesababisha ukosefu wa amani; vitendo ambavyo vinakinzana wazi na lengo la Tuzo ya Amani ya Nobel. 

Kwa nini Trump amekosa Tuzo ya Amani ya Nobel?

Jorgen Watne Frydnes, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Nobel akitangaza mshindi wa tuzo hiyo

Nina Graeger, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Oslo amesema kuhusiana na suala hili kwamba: "Orodha ya vitendo vya Trump ambavyo haviendani na malengo ya Tuzo ya Amani ya Nobel ni ndefu sana." Trump ameiondoa Marekani katika taasisi na mikataba ya pande kadhaa ya kimataifa, ameanzisha vita vya kibiashara dhidi ya washirika na maadui wa Marekani, ametishia kuitwaa Greenland kutoka Denmark, alituma askari wa gadi ya taifa katika miji mbalimbali ya Marekani na kushambulia uhuru wa vyuo vikuu na uhuru wa kujieleza.

Pamoja na haya yote, Trump alitamani sana kutunikiwa tuzo hiyo. Mashinikizo yake ya kutunukiwa Tuzo ya Nobel yalitokana na matamanio binafsi na hamu yake kubwa ya kupata umaarufu badala ya kutokana na changamoto za kibinadamu. Katika hotuba zake wakati wa uchaguzi na jumbe zake anazotuma katika mitandao ya kijamii, Trump amejiarifisha mara kadhaa kama "Mleta Amani Mkuu" na hata kuitaka hadharani Kamati ya Tuzo ya Nobel imteue kama mshindi. Kuhusiana na hili, hata baadhi ya vyombo vya habari vya kihafidhina vilianzisha kampeni za kuunga mkono ugombea wa Trump, na serikali ya Marekani kuendesha kampeni kubwa za lobi za ushawishi ili kushinda tuzo hiyo. 

Hata hivyo Kamati ya Nobel imepinga mashinikizo yote haya katika hatua mahsusi. Ingawa Tuzo ya Amani ya Nobel huko nyuma ilifanya chaguzi zilizoibua mijadala na ukosoaji mkubwa,  kuanzia kwa Kissinger hadi Umoja wa Ulaya; lakini kwa upande wa Trump, mipaka ya kimaadili na kisiasa ilikuwa kwamba, kama Donald Trump angetangazwa mshindi hatua hiyo ingehesabiwa kuwa sawa na kusambaratika kikamilifu itibari ya tuzo hiyo. 

Ni wazi kuwa, kuondolewa Trump kwenye orodha ya shakhsia walioarifishwa kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel si ishara ya uadilifu na kutoegemea upande wowote waandaaji wa Tuzo ya Amani ya Nobel, bali ni uthibitisho wa ukweli kwamba hata katika michezo ya kisiasa, vigezo vya chini kabisa vinapasa kuzingatiwa.

Your Comment

You are replying to: .
captcha