Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Mwenyekiti wa JMAT–TAIFA, Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum amesisitiza kuwa upendo na mshikamano ni nguzo kuu za kujenga amani ya kweli na ya kudumu katika taifa. Amesema kuwa jamii inayojengwa juu ya misingi ya kupendana na kusaidiana huwa na uhusiano mzuri kati ya watu wake, jambo linaloimarisha amani na kupunguza migogoro.
Akizungumza kuhusu msingi wa amani, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania alibainisha kuwa amani ya kweli huanzia katika mahusiano mema yanayojengwa kwa kujali, kuthaminiana na kusaidiana. Alieleza kuwa kitendo cha kusaidiana huondoa chuki na uhasama, kwani mtu anaposaidiwa huhisi kukubalika na kuheshimiwa, hali inayojenga imani na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Amefafanua kuwa hali hii hujitokeza wazi katika ngazi ya jamii, kama vile vijiji na mitaa, ambako wananchi wanaposhirikiana katika shughuli za maendeleo kama usafi wa mazingira, ujenzi wa miundombinu au kuwasaidia wenye mahitaji maalumu, hujenga umoja unaopunguza migogoro na kuimarisha heshima ya kudumu baina yao.
Aidha, Mwenyekiti wa JMAT–TAIFA alisisitiza kuwa amani ya taifa huanzia katika familia. Alisema kuwa kusaidiana kati ya wazazi na watoto huimarisha upendo na hupunguza migogoro ya kifamilia, na kwa kuwa familia ndiyo msingi wa jamii, mshikamano wa nyumbani huchangia moja kwa moja amani ya jamii na taifa kwa ujumla.
Akihitimisha, Mwenyekiti huyo wa JMAT-TAIFA alitoa wito kwa wananchi wote kuendeleza utamaduni wa kupendana, kusaidiana na kuthaminiana, akisisitiza kuwa kusaidiana ni nguzo muhimu ya amani kwa sababu hujenga upendo, umoja na heshima. Alisema: “Tukisaidiana kwa dhati na kwa moyo mmoja, tutajenga amani imara na ya kudumu kwa nchi yetu.”
Your Comment