19 Machi 2011 - 20:30

Mamufti wa Jordan wametoa fatuwa ya kuharamisha filamu zinazoonyesha sura ya Imam Hassan na Hussein (as).

ABNA-Mamufti wa Jordan wametoa fatuwa ya kuharamisha filamu zinazoonyesha sura ya Imam Hassan na Hussein (as).

Gazeti la al Qabas linalochapishwa Kuwait limeandika kuwa Ofisi ya Fatuwa ya Jordan imesema katika fatuwa hiyo kwamba ni haramu kuonyesha sura ya Mitume wa Mwenyezi Mungu, Masahaba wa Mtume (saw) na Ahlubaiti zake (as) katika filamu na michezo ya televisheni.

Fatuwa hiyo imetolewa kufuatia uamuzi uliochukuliwa na televisheni za MBC na Rotana za Saudi Arabia wa kutengeneza filamu ya Imam Hassan na Hussein (as) inayodhihirisha sura za watukufu hao.

Awali al Azhar huko Misri, Jumuiya ya Fiqhi ya Kiislamu na maulamaa wa Kishia pia walitoa fatuwa wakiharamisha kuonyeshwa picha na filamu zinazodhihirisha sura za Mitume wa Mwenyezi Mungu na Masahaba na Jordan tayari imepiga marufuku kuonyeshwa filamu ya Imam Hassan na Hussein katika televisheni ya nchi hiyo.

Filamu hiyo ilianza kutengenezwa mwaka jana nchini Jordan kwa ushirikiano wa Syria, Kuwait, Lebanon na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Lengo la filamu hiyo iliyopewa jina la "al Asbat" ni kuhujumu madhehebu ya Shia na kuwatetea watawala dhalimu hususan Muawiya bin Abi Sufiyan na Yazid bin Muawiya waliowaua wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Hassan na Hussein (as).