Fadhila za Sayyidna Ali bin Abi Twalib a.s
HADITHI YA AWALI: "Kwa hakika Ali ni mwingi wa huruma na upole"
Shaabi anaeleza kuwa safari moja Abu Bakr alimwona Ali akija mbele yake. Abu Bakr akatamka kuwa yeyote apendaye kufurahi kumwona mtu aliye karibu sana na Mtume ((S.a.w)) aliye na daraja kubwa, aliyetaabika sana kwa ajili ya dini ya Mwenyezi Mungu na aliye bora mbele ya Mtume kuliko yeyote mwingine, basi anapaswa kumwangalia Ali ibn Abi Talib." Akaendelea kusema kuwa amemsikia Mtume ((S.a.w)) akisema: "Kwa hakika Ali ni mwingi wa huruma na upole".
HADITHI YA PILI "Ewe Abu Huraira! Hujui kuwa mkono wangu na mkono wa Ali ni sawa katika Uadilifu?" Omar Ibn Al-Khattab amesema kuwa yeye alielezwa na Abu Bakr kwamba Abu Hureira alikwenda kwa Mtume ((S.a.w)) na akakuta gao la tende mbele yake. Akamtolea salamu Mtume ((S.a.w)) ambaye akamjibu na kumpa gao moja la tende. Alipohisabu akakuta tende 43. Baadaye akaenda kwa Ali Ibn Abi Talib ambaye pia akampa tende na alipozihisabu aliona kuwa idadi ilikuwa ile ile.
Jambo hilo likamshangaza sana. Akarejea kwa Mtume ((S.a.w)) na kumweleza yale yaliyotokea. Mtume ((S.a.w)) akatabasamu na kusema kuwa, "Ewe Abu Hureira hujui kuwa mkono wangu na mkono wa Ali ni sawa katika uadilifu?" 15
HADITHI YA TATU "Mtume na Ahlul Kisaa"
Zaidi Ibn Yathee amekariri kuwa amemsikia Abu Bakr akisema kuwa alimwona Mtume ((S.a.w)) amekaa katika hema akiegemea upinde wa Kiarabu. Pamoja naye walikuwa Seyyidna Ali (A.S.), Seyyidati Fatima (A.S.) Seyyidna Hassan na Seyyidna Hussein (A.S.). Mtume ((S.a.w)) akatamka, "Enyi Waislamu, mimi nina amani na wale wanaokaa na amani na watu walio katika hema hili na ninapigana na wale wanaopigana nao. Pia ninawapenda wale wanaowapenda na nina uadui na wale wenye uadui nao. (Kadhalika) ni mtu yule tu aliye mwema na mwenye hadhi na aliyezaliwa kwa wema ndiye atakayewapenda hao na ni yule tu mwenye kizazi kibaya ndiye atakayewabughudhi hao."
Mtu mmoja akamwuliza Zaid, "Ewe Zaid, ulimsikia Abu Bakr akisema hivyo?" Akajibu kuwa "Naapa kwa jina la Mola wa Kaaba (kuwa nimesikia)". Hadithi hii ni mashuhuri kwa jina la HADITHUL-KISAA. Hadithi hiyo imepokewa kwa njia mbalimbali kutoka kwa wanazuoni wengi wa Kishaafy, Hanafy na wengineo.
HADITHI YA NNE:Kumepokewa hadithi kutoka kwa Umar bin Khattab ambaye amesema "Nimemsikia Mtume ((S.a.w)) akieleza sifa tatu za Ali ambazo miye ningetamani kuwa na walau moja kati ya hizo. Wakati wa kueleza hadithi hiyo tulikuwepo mimi, Abu Ubaida, Abu Bakari na kikundi cha Masahaba wa Mtume ((S.a.w)). Mara Mtume ((S.a.w)) akampiga Ali begani na akatamka: 'Ewe Ali, wewe ndiye wa kwanza katika walioamini na mwanzo katika waliosilimu na kwangu miye daraja yako mithili ya Harun kwa Musa a.s."
HADITHI YA TANO: "Kumpenda Ali ni kumpenda Mtume"
Imesimuliwa hadithi kutoka kwa Ibnu Abbas kuwa Umar bina Khattab alikuwa akisema, "Jizuieni na kumtaja (kwa ubaya) Ali bin Abi Talib; hakika mambo mengi nimeyaona kwake kutoka kwa Mtume natamani ningalikuwa nalo moja tu katika ukoo wa Al-Khattab ingekuwa bora kwangu kuliko kuvipata vitu vyote vinavyopata mwangaza wa jua. Nilikuwa mimi na Abu Bakr na Abu Ubaida pamoja na baadhi ya masahaba wa Mtume, tukaenda mpaka mlangoni kwa Ummu Salama, Ali alikuwa amesimama mlangoni, tukamwambia tunamtaka Mtume ((S.a.w)). Akasema anakuja. Akatoka Mtume ((S.a.w)) tukaenda kwake.
Mtume akamwegemea Ali bin Abi Talib, kisha akampiga begani (Ali) na kusema, "Wewe ni wa kwanza kuamini miongoni mwa walioamini, mwenye maarifa ya Neema za Mwenyezi Mungu, mwenye kutekeleza ahadi za Mungu, mwadilifu katika ugawaji, mpole mno kwa raia, mbora wao mno katika kuvumilia taabu, msaidizi wangu, utakayeniosha, utakayenizika, utakayetangulia katika mambo yote ya shida (magumu) na machungu, hutarudia ukafiri baada yangu, wewe utakuwa mbele yangu na umeshika mikononi 'Liwaul-Hamad', utawafukuza watu (wasiokupenda) kwenye hodhi (Kauthar) yangu". Kisha Ibnu Abbas akasema, "Hakika Ali amefuzu kwa kuwa ni mkwe wa Mtume ((S.a.w)) na kuwa mbora katika familia yake na mkarimu wa kusaidia katika jambo lolote la kheri, mjuzi wa Qurani, mjuzi wa maana za Qurani, kuliko wengine".
HADITHI YA SITA: "Udugu kati ya Mtume na Ali"
Imepokewa hadithi kuwa Umar bin Khattab amesema kuwa Mtume ((S.a.w)) alipofunga udugu kati ya masahaba zake, akasema huyu Ali ni ndugu yangu katika dunia na akhera na Khalifa wangu kwa watoto wangu na Wasii wangu kwa umati wangu, na mrithi wa elimu yangu na ndiye mlipaji wa deni langu, mali yake ni yangu, na mali yangu ni yake, nafuu yake ni nafuu yangu, madhara yake ni madhara yangu; atakayempenda Ali hakika amenipenda mimi, na atakayembughudhi Ali hakika amenibughudhi mimi."
HADITHI YA SABA "Ali ni bora kuliko Masahaba wote"
Amehadithia Umar bin Khattab kwamba siku moja tulikuwa tumekaa katika duara na alipita Salman al-Farsi akienda kumwangalia mtu fulani. Kati yetu mmoja akasema, "Laiti mngependa nikujulisheni nani aliye bora wa umma huu baada ya Mtume wake, na aliye bora kuliko hawa watu wawili Abu Bakr na Umar?" Salman aliposimama kutaka kuondoka, akaulizwa: "Ewe Aba Abdallah unasemaje? Naye akasema, "Niliingia kwa Mtume ((S.a.w)) wakati yumo katika sakaratil mauti na nikamwuliza, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, umeshausiya?" "Akasema, huwajui waliousiwa?" (ewe Salman). Nikasema "Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua" Akasema, "Hakika Adam alimwusia (wasii wake) Shithi, hivyo alikuwa bora kuliko watoto wake wote baada yake. Nuhu alimuusia (wasii wake) Saam ambaye alikuwa bora baada yake. Musa akamusia Yusha, ambaye alikuwa bora baada yake. Suleiman akamwusia (wasii wake) Aasif Bin Barkhiya naye alikuwa bora baada yake. Isa akamwusiya Sha'muni As-Safaa ambaye alikuwa bora baada yake, na mimi nimemwusia (wasii wangu) Ali, ambaye ni mtu bora kuliko wote nitakayemwacha baada yangu".
HADITHI YA NANE: "Ali ni mjuzi bora wa hukumu za Sharia"
Katika kitabu cha Ibnu Hajar Ash-Shafiiy 22 katika mlango ambamo ametaja sifa za Masahaba amemsifu Ali (A.S.) kwa kusema kuwa Ibnu Saadi ameeleza hadithi katika "Tabakati" aliyoipokea kutoka kwa Abi Hurairah akasema kuwa "Umar Bin Khattab amesema kuwa Ali ni mwenye kujua hukumu na maamrisho ya sheria kuliko sote. Mahala pengine Umar Bin Khattab (R.A.) amesema, "Ali Bin Abi Talib ndiye mwenye ujuzi zaidi wa hukumu, sheria na maamrisho ya Mwenyezi Mungu kuliko maswahaba wote.
HADITHI YA TISA: "Omar Ibn Khattab akiri ubora wa Ali"
Omar bin Khattab (r.a.) amesema: "Najua kuwa Ali (a.s.) anayo mambo matatu, ambayo ningekuwa na mojawapo tu mimi, kati ya mambo hayo ningeona fakhari zaidi kuliko kupata ngamia wekundu. Jambo la kwanza ni kuwa Mtume (((S.A.W)).W) amemwoza Binti yake, na amemzalia mabwana wawili wa vijana wa watu wa Peponi: Hassan na Husain (A.S.) Na jambo la pili ni kufungwa milango yote isipokuwa mlango wake (yaani, Mtume (((S.A.W)).W) aliifunga milango yote iliyokuwa ikipitiwa na Masahaba kama vile Abu Bakar, Omar bin Khattab na wengineo kutoka majumbani mwao kuingia Masjidun-Nabawy. Na jambo la tatu ni kuwa Mtume (((S.A.W)).W) alimpa bendera siku ya vita ya Khaybar.
HADITHI YA KUMI:"Ali ni bora kuliko wote baada ya Mtume ((S.a.w))"
Katika "Yanabiul-Mawaddah" imepokewa hadithi kwa Sayyid All Hamdaniy Shafiiy, kutoka kwa Ibnu Omar ambaye anaeleza kwamba Mtume ((S.a.w)) amesema, "Bora wa wanaume wenu ni Ali Bin Abi Talib, na bora wa vijana wenu ni Hasan na Husein na bora wa wanawake wenu ni Fatimah binti Muhammad ((S.a.w))"
Wanazuoni wa Kisunni wamekariri hadithi hii au yenye maana kama hii katika vitabu vyao vingi kama vile Ali Al-Muttaqi Al-Hanafii katika Kanzul-Ummal (juzu ya 6), ya kutoka kwa Ibnu Abbas akisema kuwa, Mtume ((S.a.w)) amesema "Ali ni bora miongoni mwa watu wote." Al-Ganji Shafiiy katika Kifaayatu-Taalib, alikariri hadithi kutokana na Jaabir Bin Abdillah, kuwa amesema, "Tulikuwa kwa Mtume ((S.a.w)) akasema, basi mara Ali Bin Abi Talib akaja; Mtume ((S.a.w)) akasema, "Hakika amekujieni ndugu yangu." Kisha akageuka kuelekea upande wa El-Kaaba akaipiga kwa mkono wake, na akasema, utNaapa kwa yule ambaye nafasi yangu ipo mikononi mwake, hakika huyu (Ali) na wafuasi wake, ndio wenye kufaulu siku ya Kiyama.
HADITHI YA KUMI NA MOJA: "Anayefarakana na Ali anafarakana na Mtume"
Katika Manaaqib ya Al-Khateeb Al-Muwaffaq bin Ahmad Al-Khwarizmi Al-Hanafi uk. 62, imo hadithi iliyotokana na Ibnu Omar kuwa Mtume ((S.a.w)) amesema. Mtu yeyote atakayefarakana (Kujitenga) na Ali atakuwa amefarakana nami na yeyote atakayefarakana nami atakuwa amefarakana na Mwenyezi Mungu mtukufu.