26 Novemba 2014 - 09:42
Marekani yaongeza askari kukabiliana na maandamano Ferguson

Askari wa kutuliza fujo wapatap 2,000 wamepelekwa ndani na karibu na kitongoji cha Ferguson, nchini Marekani ili kukabiliana na wananchi wenye hasira kali wanaodai haki itendeke.

Askari  wa kutuliza fujo wapatap 2,000 wamepelekwa ndani na karibu na kitongoji cha Ferguson, nchini Marekani ili kukabiliana na wananchi wenye hasira kali wanaodai haki itendeke.

 Maandamano yalizuka baada ya jopo la wazee wa baraza la mahakama kuamua kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha ili kumfungulia mashtaka polisi mweupe kuhusiana na tukio la mwezi Agosti ambapo alimpiga risasi na kumuua kijana mweusi Michael Brown ambaye hakuwa na silaha na alinyoosha mikono kujisalimisha lakini alipigwa risasi na kuuawa. Kulikuwa na maandamano ya kupinga uamuzi huo katika miji kadhaa ya Marekani, ikiwemo New York na Washington.

Rais Barack Obama amelaani vitendo vya uharibifu na uporaji mali ambavyo alisema ni vya kihalifu na waliohusika wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Alitoa wito wa kuwepo mazungumzo kuhusiana na suala la utekelezwaji wa sheria nchini Marekani. Obama alisema "Kwa wale wanaodhani kilichotokea Ferguson ni sababu ya kuzusha machafuko, sina huruma yoyote kuhusu hilo. Sina huruma kabisa kwa kuharibu jamii zenu wenyewe. Lakini kwa watu wengi ambao wanahisi uchungu, kwa sababu wanaona kuwa huenda baadhi ya jamii hazitendewi haki au baadhi ya watu hawaonekani kuwa sawa na wengine, hilo naelewa. Na nataka kufanya kazi nanyi na nataka kusonga mbele nanyi".

 Mwanasheria mkuu Eric Holder aliahidi kuwa uchunguzi wa serikali kuhusiana na kisa cha mauaji ya Brown utafanywa kwa wakati unaofaa. "Ipo haja ya kuwaleta watu pamoja. Huu ni wakati mgumu. Kwa watu wa Ferguson na ni wakati mgumu kwa watu wa nchi hii. Nadhani ni fursa ya sisi kutafuta vitu vinavyotuleta pamoja kama taifa. Kuwa wakweli miongoni mwetu kuhusu mambo hayo yanayoendelea kutugawanya na kutafuta mbinu za kuufanya muungano huu kuwa bora zaidi"

Wilson, ambaye angekabiliwa na mashtaka ya mauaji au kuua bila kukusudia, ameiambia televisheni ya Marekani ya ABC News kuwa hakuna chochote angefanya tofauti wakati wa makabiliano yake na Brown ambacho kingezuia kifo cha kijana huyo. Alisema hajutii kitendo hicho kwa sababu anajua alifanya jambo la kweli kulingana na mazingira aliyokuwamo, akiongeza kwamba angefanya hivyo hivyo hata kama Brown angekuwa mweupe.

Nakala zilizotolewa na waendesha mashtaka zilisema kuwa Wilson ambaye alipewa likizo ya lazima baada ya tukio hilo, aliliambia jopo la wazee wa baraza la mahakama kuwa Brown alijaribu kumpokonya bastola yake, na kuwa ofisa huyo akahisi maisha yake yalikuwa hatarini wakati akifyatua risasi.

Maandamano yalisambaa kutoka Los Angeles hadi Washington. Mjini New York, polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuudhibiti umati baada ya waandamanaji kujaribu kuzifunga barabara. Katika majimbo ya Oklahoma, California na Atlanta, waandamanaji walizuia magari, wakati pia mjini Boston kukishuhudiwa maandamano.

Suala la ubaguzi wa rangi nchini Marekani linasadikiwa kuwa ni tatizo la muda mrefu lisilo na ufumbuzi.

waandamaji wenye hasira kali wakilihujumu gari la polisi

Tags