11 Desemba 2014 - 19:33
Radi amali za viongozi mbali mbali kuhusu mateso ya gereza la Guantanamo

Mateso yanayofanywa na serikali ya marekani dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi walioko katika gereza la Guantanamo imeonekana kuwa ni unyama wa hali ya juu na ukiukaji wa haki za binadamu, viongozi wengi duniani wamesikitishwa sana na ukatili huo unaofanya na serikali ya Marekani.

Mateso yanayofanywa na serikali ya marekani dhidi ya watuhumiwa wa ugaidi walioko katika gereza la Guantanamo imeonekana kuwa ni unyama wa hali ya juu na ukiukaji wa haki za binadamu, viongozi wengi duniani wamesikitishwa sana na ukatili huo unaofanya na serikali ya Marekani.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ameungana na viongozi wengine kukemea vikali mbinu za mateso zilizotumiwa na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) kwa washukiwa wa ugaidi kufuatia kuchapishwa ripoti maalum.

Cameron amesema mateso hayo yalioonekana kufanyiwa washukiwa hao wa kundi la kigaidi la Alqaida ni makubwa kuliko yalivyodhaniwa.

"Wacha tuwe wa wazi kabisa, mateso ni makosa, kutekeleza visa vya mateso ni makosa makubwa," alisema Cameron alipokutana na waandishi habari mjini Ankara, Uturuki, ambapo alikuwa ziarani kukutana na maafisa wa nchi hiyo kujadili ushirikiano wa usalama katika kupambana na vitisho vya ugaidi kutoka kwa kundi la kigaidi la Daesh.

Cameron amesema yalioyoangaziwa katika ripoti hiyo ya kurasa 500 iliyotolewa na wachunguzi wa baraza la Seneti la Marekani ni uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu katika kupambana na ugaidi.

 Aidha wakosoaji wa ripoti hiyo nchini Uingereza wameitaka serikali ya Marekani kujitokeza wazi na kusema jukumu lake katika kuwasaidia maafisa wa shirika hilo la ujasusi kukabiliana na ugaidi, ambapo magaidi walipelekwa katika maeneo ya siri na kuteswa na maafisa waliowahoji.

Ripoti hiyo iliyofichua mateso hayo imesema washukiwa wengi walinyanyaswa vibaya na kwamba magereza ya siri ya CIA yaligeuka kuwa vyumba vya mateso. Ripoti hiyo imeendelea kusema kwamba mbinu hizo za kikatili hazikuchangia kwa aina yoyote ile kuifanya Marekani kuwa nchi salama zaidi baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001.

Hata hivyo, Rais Barrcak Obama amesema umuhimu wa kutolewa kwa ripoti hii ni nchi hiyo kujifunza kutokana na yaliyotokea na watu kuelewa ni kwa nini alipiga marufuku masuala kama haya kama hatua ya kwanza wakati akiingia madarakani.

  Kwa upande mwengine, Korea ya Kaskazini ambayo imekuwa ikilaumiwa mara kwa mara na Marekani kufuatia uvunjifu wa haki za binaadamu, nayo imepaza sauti kuhusu ripoti hii kwa kulihimiza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani mateso yaliyofanywa na Marekani kwa washukiwa wa ugaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema ripoti hii ni mtihani mkubwa sana wa kupima uaminifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Msemaji huyo amesema, kwa kuzungumzia rikodi ya masuala ya haki za binaadamu ya Korea ya Kaskazini na kufumbia macho mambo yaliyobainika kufanywa na mwanachama wake wa kudumu ambaye ni Marekani, kutaonesha wazi kwamba Baraza hilo lipo tu na halina makali yoyote.

Huku hayo yakiarifiwa, China imeitaka Marekani kurekebisha mienendo yake baada ya baraza la Seneti kusema katika ripoti yake kwamba CIA iliipotosha ikulu ya Marekani pamoja na umma juu ya mateso kwa washukiwa wa ugaidi.

Hata hivyo, shirika hilo la kijasusi limekanusha madai ya ripoti hiyo.

Weledi wa mambo wanasema kwamba pamoja na kwamba ripoti hiyo imeandikwa na wamarekani na kwamba wanachunga maslahi ya nchi yao kwa kupunguza ukali wa ripoti hiyo, lakini bado ripoti hiyo inaakisi na kuashiria sehemu tu ya mateso yanayojiri katika gereza hilo lenye kila aina ya unyama na unyanyasaji.

 

 

Tags