24 Februari 2019 - 07:55
Urusi, China zaonya dhidi ya uvamizi Venezuela

Ikumbukwe kuwa nchini Ufaransa na Hispania kuna maandamano wananchi wanapinga serikali zao lakini hakuna nchi yeyote ya Ulaya iliyounga mkono wapinzani au hata kuwapelekea silaha wananachi ili waziangushe serikali zao.

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Urusi na China zinasema kuna uchokozi wa makusudi unaofanywa  na Marekani na washirika wake dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela, huku zikitoa wito dhidi ya uingiliaji kati kijeshi au hatua zozote za kuugeuza mzozo huo kuwa vita.

China imetamka hadharani hivi ikipinga hatua yoyote inayoweza kuzusha ghasia na machafuko nchini Venezuela. msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Geng Shuang, amesema nchi yake inafahamu kuwa pamekuwepo na hatua za makusudi za uchokozi dhidi ya serikali ya Venezuela, licha ya serikali hiyo kujizuwia kujibu uchokozi huo.

"Tumeona kwamba kipindi sasa serikali ya Venezuela imejizuwia na imejitolea kudumisha amani na utulivu wa ndani ya nchi, hali ambayo imewezesha kuzuwia umwagaji damu mkubwa. Lakini kama kile kinachoitwa misaada ya kibinaadamu ya Marekani kitalazimishwa kuingia ndani ya Venezuela, ni wazi kuwa kutazuka machafuko yatakayokuwa na matokeo mabaya kabisa," alisema Shuang, akiongeza kuwa nchi yake inapingana na uingiliaji kati kijeshi dhidi ya Venezuela na pia inakataa vitendo vyovyote ambavyo vitachochea machafuko.

Kauli kama hii imetolewa pia na Urusi, ambayo nayo kupitia msemaji wake wa mambo ya kigeni, Maria Zakharova, imesema inafahamu kuwa Marekani inaandaa uchokozi ikitumia kanuni za hali ya juu za sayansi ya kijeshi.

"Vikosi maalum vya jeshi la Marekani na vifaa vinatumwa karibu sana na mpaka wa Venezueal. Kuna taarifa kwamba kampuni za Kimarekani na washirika wao wa Jumuiya ya NATO wananunuwa kiwango kikubwa cha silaha kutoka moja ya nchi za Ulaya Mashariki kwa ajili ya kuwafikishia wapinzani ndani ya ardhi ya Venezuela," alisema Zakharova, akiongeza kuwa kile kinachoitwa misaada ya kibinaadamu inayopangwa kuingizwa nchini Venezuela mwanzoni mwa mwezi ujao wa Machi, kitakuwa ni sehemu ndogo tu ya matumizi ya kibinaadamu, huku sehemu kubwa zikiwa zana za kijeshi.

Haya yanakuja huku Marekani ikiimarisha shinikizo lake dhidi ya serikali ya Venezuela, nayo serikali ya Rais Maduro ikiamuru kufungwa mpaka kati ya nchi hiyo na Brazil. 

Kwenye hotuba yake ya mwanzoni mwa wiki kwa jamii ya Wavenezuela wanaoishi nchini Marekani, Rais Donald Trump alisema Marekani inataka pawepo na ukabidhianaji wa amani wa madaraka nchini Venezuela lakini hakuondosha uwezekano wa hatua za kijeshi.

Ikumbukwe kuwa nchini Ufaransa na Hispania kuna maandamano wananchi wanapinga serikali zao lakini hakuna nchi yeyote ya Ulaya iliyounga mkono wapinzani au hata kuwapelekea silaha wananachi ili waziangushe serikali zao.

291

Tags