(ABNA24.com) Sadiq al-Mahdi, kiongozi wa Hizb al-Umma al-Qawmmy amesema kuwa, Serikali ya Mpito ya Sudan inakabiliwa na changamoto ambazo kama itashindwa kuzipatia ufumbuzi basi itakuwa imejichimbia kaburi.
Kiongozi huyo mkongwe wa upinzani nchini Sudan ametahadharisha kuhusua anga ya kisiasa inayotawala hivi sasa nchini humo na udhaifu wa Serikali ya Mpito ya katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi hiyo.
Mwanasiasa huyo amesema kuwa, Serikali ya Mpito ya Sudan inakabiliwa na changamoto nyingi kama kuboresha hali mbaya ya uchumi, mwenendo wa amani na makundi ya wabeba silaha na kurejesha amani na uthabiti wa nchi
Sadiq al-Mahdi ameongeza kuwa, changamoto nyingine nisiasa za madola ajinabi za kutumia vibaya fursa na njama zenye lengo la kurejesha mfumo wa kisiasa wa enzi za utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.
Katika miezi ya hivi karibuni shakhsia huru nchini Sudan wamekuwa wakitahadharisha kuhusiana na kuendelea uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ambapo Saudia ni moja ya nchi zinazoonyeshwa kidole cha lawama.
Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani Rais Omar al-Bashir na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda baraza la kijeshi ambalo nalo lilivunjwa na kuundwa Baraza la Utawala wa Mpito.
/129