9 Oktoba 2022 - 19:59
Jeshi la Somalia: Vita dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabab vitaendelea

Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, vita dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabab vitaendelea hadi pale litakapofanikiwa kulitokomeza kikamilifu kundi hilo linalofanya mauaji.

Taarifa ya jeshi la Somalia imesisitiza kuwa, jeshi la nchi hiyo liko katika vita dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab na kwambba, vita hivyo vitaendelea mpaka litakapofanikiwa kung'oa kabisa mizizi ya kundi hilo la kigaidi.

Taarifa hiyo ya jeshi inatolewa siku moja tu baada ya jana kutangazwa kuwa, wanamgambo 14 wa kundi la kigaidi la al-Shabab wameangamizwa akiwemo kiongozi wao muhimu kufuatia operesheni ya jeshi kusini mwa nchi hiyo.

Vikosi vya usalama vya Somalia vimetangaza kupata mafanikio makubwa katika wiki za hivi karibuni dhidi ya genge la ukufurishaji la al Shabab limejitangaza kuwa ni tawi la mtandao wa kigaidi wa al Qaeda. Serikali ya Somalia imesema kuwa, imepata mafanikio hayo kwa kupigana bega kwa bega na vikundi vya kujilinda vya kkieneo ambavyo vimechoshwa na jinai na mauaji ya kundi la al Shabaab.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

 

Genge la kigaidi la al Shabaab limekuwa likijaribu kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007.

Al-Shabaab walifukuzwa Mogadishu na Jeshi la Somalia na vikosi vya Umoja wa Afrika mwaka 2011, hata hivyo, kundi hilo la kigaidi bado linadhibiti maeneo makubwa ya vijijini nchini humo.

342/