Luteka hiyo inayoonyesha uwezo wa ulinzi wa nchi kwa kawaida hufanyika kila mwaka au dharura inapotokea.
Msururu wa maneva za pamoja za "Zulfiqar" za Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika pwani ya Makran huimarisha usalama wa mipaka ya bahari ya kusini mwa nchi na kuongeza kina cha kistratijia cha Iran kutoka Bahari ya Oman na maeneo ya mbali zaidi ya bahari hiyo.
Katika mazoezi ya pamoja ya "Zulfiqar 1401", kikosi cha askari wa kutembea kwa miguu, vifaru na magari ya deraya, mifumo ya ulinzi, manowari, nyambizi na helikopta zimekuwepo katika eneo la jumla la mazoezi hayo ya siku kadhaa na ambayo yalianza rasmi Ijumaa asubuhi.
Hatua hizi zinachukuliwa kwa kuzingatia mazoezi ya kila mwaka na kwa msingi wa kalenda, kuimarisha mafunzo na utayari wa kupambana pamoja na kutekeleza baadhi ya mipango ya kioparesheni na kiintelijensia ili kuboresha usalama wa kikanda.
Moja ya nukta mashuhuri katika zoezi hili ni utumiaji wa zana na silaha zilizoundwa kikamilifu ndani ya Iran. Silaha hizo zimeundwa na kuzalishwa kwa kutegemea viwanda vya ulinzi vya Iran na pia kampuni za Iran zenye msingi wa kielimu.
"Admeri Habibullah Sayari" kamanda wa mazoezi ya kijeshi ya Zulfikar 1401 amesema: Kati ya jumbe za zoezi hili ni kufanya vikwazo vya silaha dhidi ya Iran visiwe na maana kwa kutumia silaha na zana zilizoundwa kikamilifu nchini Iran na hatimaye kuonyesha mamlaka na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika miaka ya hivi karibuni, na licha ya vikwazo hivyo, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limefanya mazoezi kadhaa katika maeneo tofauti, ambayo yamekuwa na matokeo muhimu katika kuongeza nguvu za kivita na kuboresha uwezo wa kujihami, kumzuia adui na kuondoa vitisho. Kufanyia majaribio silaha na zana zilizotengenezwa nchini Iran, zikiwemo meli za kivita na nyambizi, makombora, ndege zisizo na rubani au drone za upelelezi na za kivita, ndege za kawaida za kivita, vifaru pamoja na kufanya mazoezi ya mbinu za mapigano ni miongoni mwa hatua zinazotekelezwa katika mazoezi hayo. Bila shaka mazoezi hayo yamekuwa na nafasi muhimu sana katika kuongeza nguvu za kijeshi za Iran.
Leo, kikosi cha wanamaji cha kimkakati cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kiko kwenye bahari za kimataifa na hukabiliana mara kwa mara na uharamia katika Ghuba ya Aden. Bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kupeperushwa na manowari za Jeshi la Iran katika Bahari Nyekundu, Bahari ya Mediterania, Bahari ya Kusini ya China, Bahari ya Hindi, na Bahari ya Atlantiki ya Kusini na Kaskazini. Uwepo wa manowari za Jeshi la Iran katika bahari za kimataifa ni ishara ya wazi ya uwezo mkubwa wa kujihami wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Jamhuri ya Kiislamu pia ni miongoni mwa nchi kubwa zaidi katika uzalishaji wa makombora na ndege zisizo na rubani duniani na ina uwezo bora zaidi wa makombora na ndege zisizo na rubani katika eneo la Asia Magharibi. Mafanikio hayo yamepatikana kwa kutumia maarifa na wataalamu wa ndani. Kwa mujibu ripoti ya hivi punde ya shirika moja la utafiti wa kijeshi la Marekani linalojulikana kama Global Firepower Iran imeorodheshwa kuwa nchi ya 14 kwa mtazamo wa nguvu za kijeshi duniani.
Ni dhahiri kwamba nchi za kieneo na nje ya kanda daima hufuatilia mazoezi ya jeshi la Iran na kuyachambua katika vyombo vyao vya habari. Kwa mfano, mashirika ya habari ya Associated Press na Deutsche Welle mwaka jana yalitaja Mazoezi ya Pamoja ya Zulfiqar 1400 ya Jeshi la Iran kuwa yaliyokuwa na lengo la kuboresha utayarifu wa kukabiliana na vitisho vya kigeni na uchokozi wowote unaoweza kutokea dhidi ya Iran. Aidha Kanali ya 12 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni pia imeyataja mazeozi hayo kuwa yaliyokuwa na lengo la kutuma ujumbe kwa Israel.
Nukta nyingine muhimu kuhusu kufanyika mazoezi hayo ni kwamba kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, udumishaji usalama unazihusu nchi zote za eneo na hilo linaweza kutekelezwa tu kwa kutegemea nguvu na umoja baina ya nchi za eneo.
Kuwepo kwa madola ajinabi katika eneo la Asia Magharibi hakusaidii usalama na utulivu wa eneo hili. Kwa hivyo, Iran daima imekuwa ikishirikiana na majirani zake, ikiwa ni pamoja na katika Ghuba ya Uajemi na ushirikiano huo ni msingi wa sera zake za nje.
"Admeri Habibullah Sayari" kamanda wa mazoezi ya kijeshi ya Zulfikar 1401 aidha amefafanua kuhusu nukta hiyo na kusema: "Ujumbe wa zoezi kubwa la Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi za eneo ni ukumbusho wa uwezo uliopo ndani ya eneo ambapo amani inaweza kupatikana tu kwa ushirikiano bila ya kuhitajika wageni. Nukta hii ni muhimu kwa sababu historia imethibitisha kwamba nchi nyingine za nje ya kanda zimekuwa zikiibua vita na ukosefu wa usalama na wala hazijaleta lolote la maana isipokuwa ukosefu wa usalama, vita na uvamizi katika eneo la Magharibi mwa Asia."
342/