Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Mei 2023

10:49:20
1362351

Guterres: Uhuru wa vyombo vya habari ni sehemu muhimu ya haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kuwa, uhuru wa vyombo vya habari ni kanuni ya demokrasia na uadilifu, na ni sehemu muhimu ya haki za binadamu.

Tarehe Tatu Mei huadhimishwa kila mwaka kama Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Siku hii ilipewa jina hilo na Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika sherehe za maadhimishio ya siku hii kwamba: Uhuru wa vyombo vya habari unashambuliwa katika kila kona ya dunia. "Ukweli unatishiwa na habari zisizo sahihi na matamshi ya chuki". Vitendo hivi vinalenga kufifisha mipaka kati ya ukweli na njozi tupu, kati ya sayansi na njama. 

Guterres ameongeza kusema kuwa:Tunakabiliwa na ongezeko la mkusanyiko wa tasnia ya habari mikononi mwa watu wachache, anguko la kifedha la mashirika mengi huru ya habari na ongezeko la sheria na kanuni za kitaifa zinazowawekea vikwazo na kuwabana  waandishi wa habari, kuongezeka kwa udhibiti na vitisho kwa uhuru wa kujieleza.  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amebainisha kuwa waandishi habari wasiopungua 67 waliuawa mwaka uliopita wa 2022; idadi ambayo imetajwa kuwa sawa na ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. Hii ni katika hali ambayo karibu robo tatu ya waandishi wa habari wanawake wamekumbwa na dhuluma mtandaoni, huku mmoja kati ya wanne akitishiwa kushambuliwa.

342/