Main Title

source : Parstoday
Jumatano

3 Mei 2023

10:50:30
1362353

Mabadiliko ya wazi katika mtazamo wa Wamarekani kuhusu utawala wa kibaguzi wa Israel

Hivi sasa kunashuhudiwa mabadiliko ya wazi katika mtazamo wa Wamarekani kuhusu utawala dhalimu wa Kizayuni kutokana na kuongezeka sana misimamo mikali na ya kibaguzi ndani ya utawala huo pandikizi. Idadi ya Wamarekani wanaoamini kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni wa kibaguzi, imeongezeka.

Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel, asili na msingi wake mkuu ni ubaguzi wa kizazi. Kwani mbali na kuwapora Wapalestina ardhi zao, kuna itikadi moja mbaya ndiyo inayotawala ndani ya utawala wa Kizayuni nayo ni ya kujiona Mayahudi ni kizazi bora kuliko watu wote duniani na huo ndio msingi wa jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina na watu wengine. 

Vitendo vya kibaguzi za Wazayuni vimeongezeka sana hivi sasa baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali zaidi ya Kizayuni inayoongozwa na waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Serikali hiyo ina watu wenye chuki za kidini na kikabila kama Itamar Ben-Gvir ambaye haoni hata haya kutangaza waziwazi chuki zake dhidi ya Waarabu. Wazayuni kama hao wanaamini kuwa Wapalesitna na Waarabu lazima wote waondoke kwenye ardhi za Palestina. Kama hilo halitoshi, serikali yenye misimamo mikali zaidi ya utawala wa Kizayuni imepasisha sheria zilizo dhidi ya Wapalestina, inafanya ukatili mkubwa dhidi ya taifa hilo linalodhulumiwa na inachukua hatua za kila namna za kuwakandamiza Wapalestina kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. 

Jinai hizo za Wazayuni zimezidisha hasira na chuki dhidi ya Israel katika eneo la Asia Magharibi na duniani kiujumla na sasa hasira hizo zinaongezeka hata ndani ya jamii ya Wamarekani. Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Maryland huko Marekani unaonesha kuwa, asilimia 20 ya wafuasi wa chama cha Republican na asilimia 44 ya wafuasi wa chama cha Democratic, wanaamini kuwa Israel ni utawala wa kibaguzi na wanaunga mkono kampeni ya kuwekewa vikwazo utawala huo wa Kizayuni.

Takwimu hizo mpya zimetolewa katika hali ambayo, lobi na makundi yenye ushawishi ya Kizayuni yana nguvu ndani ya muundo wa utawala wa Marekani kiasi kwamba jamii ya nchi hiyo haina uhuru wowote mkubwa wa kutoa maoni yake kuhusu utawala wa Kizayuni. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika kwenye Twitter: Ni jambo lililo wazi kwamba kama Wamarekani watapewa uhuru wa kutosha wa kutoa maoni yao kuhusu Wazayuni na lau kama lobi na makundi ya Kizayuni hayangekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya muundo wa utawala wa Marekani, basi tungeona maajabu ya idadi kubwa ya wananchi wa Marekani wanaochukizwa na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Suala jingine la kuligusia hapa ni kwamba, ijapokuwa serikali ya Marekani ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni, lakini hivi sasa misimamo imeanza kubadilika hata ndani ya muundo wa utawala wa Marekani. Wafuasi wa chama cha Democratic huko Marekani, muda wote wana matatizo na mrengo wa kulia wa Israel. Hatua za siasa kali kupindukia na za kibaguzi za serikali mpya ya Israel zimepelekea kushuhudiwa upinzani na ukosoaji mkubwa kutoka hata ndani ya serikali Marekani.  

Licha ya kupita miezi minne ya tangu kuingia madarakani serikali mpya ya utawala wa kizayuni ya Benjamin Netanyahu, lakini serikali ya Marekani haijaonesha nia ya kumkaribisha nchini humo waziri mkuu huyo wa Israel. Shirika la habari la Reuters limeandika: Tangu mwishoni mwa muongo wa 1970 hadi hivi sasa, mawaziri wakuu wa Israel walikuwa wanaalikwa kutembelea Marekani katika wiki za awali kabisa za kuingia madarakani na kuonana na rais wa Marekani. Hadi hivi sasa ni mawaziri wakuu wawili tu kati ya 13 wa Israel hawajafanyiwa hivyo na Marekani.

Siasa kuu za serikali ya hivi sasa ya mrengo wa kulia ya Israel, ni kuongeza kasi ya kupora ardhi za Wapalesina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni pamoja na kufanya mabadiliko makubwa ya sheria za utawala wa Kizayuni. Maafisa mbalimbali wa Marekani wamekuwa wakilalamikia waziwazi siasa hizo kali kupindukia za Wazayuni. David Makovsky, mshauri wa ngazi za juu wa zamani na mwakilishi maalumu wa Marekani katika mazungumzo kati ya Israel na Palestina ameandika: Ujumbe wa wazi kabisa ambao viongozi wa Marekani wanataka kuipa Israel ni kwamba, kama viongozi wa Israel wataendelea na siasa zao za hivi sasa, basi wasitarajie kabisa kukaribishwa katika (Ikulu ya Marekani), White House. 

342/